Habari za leo rafiki yangu?

Karibu tena kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto ambapo tunapata nafasi ya kushauriana kuhusiana na changamoto mbalimbali tunazopitia katika safari yetu ya mafanikio.

Leo tunakwenda kushauriana kuhusu mambo ya kuzingatia kama unataka kurudi shuleni ili kukamilisha ndoto kubwa za maisha yako.

Ukweli ni kwamba, kila mmoja wetu ana ndoto kubwa kwenye maisha yetu, kila mtu ana kitu ambacho kinamsukuma zaidi ya vitu vingine. Na muhimu zaidi, kila mmoja wetu ana kusudi la kuwa hapa duniani. Japo ni wachache sana wanaoyajua mambo haya, lakini wale wanaoyajua wanakuwa na maisha bora sana.

Sasa pamoja na kuwa na ndoto kubwa na kusudi la maisha, changamoto za maisha zinaweza kuingilia katikati, zikakatisha ile njia ya kuelekea kwenye ndoto kubwa. Hapa wengi huona ndoto hizo haziwezekani tena, lakini wapo wachache ambao hawakubali ndoto zao zife.

Hawa ndiyo wanaochukua hatua kuhakikisha wanafanyia kazi ndoto zao, hata kama muda umekwenda.

Moja ya maeneo ambayo watu hukatisha ni kwenye elimu. Labda kwa kutokufaulu kwa kiwango ambacho kinampa mtu nafasi ya kusoma kile anachopenda, au kukosa fedha ya kulipa ada ili kuendelea na masomo. Wengi wanapokutana na changamoto hizi kwenye elimu hukubali kuachana na ndoto zao na kukubali yale maisha yanayopatikana.

kurudi shule

Lakini wapo ambao wanakutana na changamoto za aina hii kwenye elimu, wanashindwa kuendelea kwa wakati ule, lakini hawafuti ndoto zao. Bali wanatengeneza mazingira bora ya kuja kutekeleza ndoto zao baadaye.

Katika makala yetu ya ushauri wa changamoto leo, tunakwenda kuangalia kundi hili la watu ambao walisimamisha ndoto zao kwa muda, lakini baadaye wanarudi kwenye kufanyia ndoto zao, hasa kwa kuanzia na kurudi shule.

Kabla hatujaingia ndani na kuangalia hatua zipi za kuchukua, tusome maoni aliyotuandikia msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

Nina umri wa miaka 22, Niliitimu shule ya msingi mwaka 2012 na nilichaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari lakini kwa bahati mbaya wazazi wangu hawakuwa na fedha ya kunisomesha. Pamoja na wazazi wangu kukosa fedha za kunisomesha niliahidi kutafuta pesa kwa hali na mali ili nije nihakikishe hiyo fedha inanisomesha na kupata moja ya kazi ambayo ni moja ya ndoto zangu tangu utotoni, Mungu si Athumani ni mwaka wa 5 sasa tangu niitimu elimu ya msingi, nimefanikiwa kupata kiasi cha shilingi milioni 12, kutokana na kufanyia vibarua vya mikono na kuanza biashara ya mazao. Sasa nimeona huu ndio muda muafaka wa mimi kwenda shule, lakini changamoto ninayo kutana nayo ni ya wazazi wangu na ndugu zangu kunizuia nisiende shule kwa madai kuwa ninaweza hata nisije kupata ajira na badala yake wananitaka niendelee na biashara. Lakini nami bado natamani kusoma ili nije nitimize moja ya ndoto zangu ! Naomba Ushauri wa mawazo, je nifuate lipi niache lipi? – Paul D. C.

Kama tulivyosoma maelezo ya msomaji mwenzetu Paul, kuna kitu kikubwa ambacho kinaonekana kuwa ndani yake.

Ni rahisi kwa nje kusema kwamba muda umekwenda na aachane na mawazo hayo ya kusoma na aendelee kutafuta fedha, maelezo haya yanaonesha kabisa kwamba hitaji la kutimiza ndoto yake kubwa bado lipo ndani yake. Halijafa kwa miaka mitano ambayo hakuwa kwenye elimu na halionekani kufa siku yoyote ya karibuni.

Hivyo ushauri wangu katika hali kama hii, ni mtu ukae chini na kujisikiliza wewe mwenyewe. Wengi watakuwa na mengi ya kusema, itakuwepo mifano mingi utakayopewa na sababu nyingi utakazopewa. Lakini mwisho wa siku, wewe ndiye unayejua zaidi kuhusu wewe kuliko mtu mwingine yeyote.

Kaa chini na jisikilize ndani yako, je kurudi shule ni kitu ambacho kweli unakihitaji na ndoto unayokazana kuifikia, je inatoka ndani yako kweli? Je ni kitu ambacho kinakunyima usingizi usiku? Je ni kitu ambacho upo tayari kukifanya kwa maisha yako yote, hata kama hakuna watakaokuwa wanakulipa kwa kufanya hivyo?

Haya ni maswali muhimu sana unayopaswa kuyajibu wewe mwenyewe ukiwa na utulivu wa kutosha.

Baada ya kuamua kwamba kweli unataka kufanyia kazi ndoto yako na unahitaji kurudi shuleni ili kukamilisha ndoto yako, hapa yapo mambo muhimu ya kuzingatia.

  1. Jiandae, safari itakuwa ngumu kuliko unavyofikiri.

Pamoja na kwamba unapenda kufikia ndoto yako, pamoja na kwamba una shauku kubwa, lakini usijiweke upofu kwa kufikiri mambo yatakuwa mteremko. Safari hii itakuwa ngumu kuliko unavyofikiri sasa. Unaweza kupanga kwamba ukienda shule utamaliza ndani ya muda, ukajikuta unafeli masomo na kulazimika kurudia tena.

Unaweza kufika wakati masomo yakawa magumu kuliko ulivyofikiri, wakati mwingine ukaonewa kwa kunyimwa ulichostahili kupata. Wakati mwingine safari itaonekana ngumu, isiyowezekana na kuona bora kuacha. Kamwe usikubali kufikia hatua hiyo ya kukata tamaa, kwa sababu utakuwa umeyavuruga maisha yako kwa kiasi kikubwa sana.

Sikuambii haya ili kukutisha na kukukatisha tamaa, bali nakuandaa na yale unayokwenda kukutana nayo. Kwa sababu wengi hujipa upofu na wanapokutana na magumu huanza kulalamika. Mimi nakuambia mapema, ili unapokutana nayo ujiambie nilijua hili, hivyo halinibabaishi.

SOMA; WAHITIMU; Mambo Kumi Muhimu Ambayo Hujawahi Kufundishwa Shuleni Na Ni Muhimu Sana Kwenye Maisha Yako.

  1. Hakikisha una chanzo cha uhakika cha kipato ili kuweza kujisomesha.

Unaporudi shule kuna vitu viwili unapaswa kuviweka kwenye elimu yako, muda na fedha. Unahitaji muda wa kusoma mpaka kuhitimu, na inaweza kuwa miaka mingi kuliko unavyofikiri. Pia unahitaji fedha za kuweza kugharamia elimu yako na hata kuendesha maisha yako.

Hapa ndipo changamoto kubwa inapoanzia, kwa sababu muda unaohitajika kwenye elimu, unafanya usiweze kuweka muda kwenye shughuli za kuzalisha kipato, hasa zile zinazotegemea nguvu zako moja kwa moja. Lakini pia muda unavyokwenda gharama za maisha zinazidi kuwa juu.

Hivyo hapa unahitaji kuwa na njia ya uhakika ya kutengeneza kipato ili safari yako iende vizuri.  Kwa kuwa Paul ameweza kufanya kazi na kuweka akiba, anaweza kuanzisha biashara ambazo anaweza kuzisimamia kwa muda anaopata, wakati anaendelea na elimu yake.

Na kila wakati, ni muhimu kuhakikisha una kiasi cha fedha kama akiba na kama fedha ya tahadhari, hizi zitawezesha kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza.

SOMA; USHAURI; Kuongeza Elimu (Ya Darasani) Siyo Njia Sahihi Kwako Kuongeza Kipato.

  1. Pangilia muda wako vizuri kuhakikisha unakamilisha masomo kwa muda unaohitajika.

Changamoto ya kurudi shule wakati umeshaendelea na maisha mengine huwa ni kuchukulia elimu kama siyo kipaumbele cha kwanza. Hivyo unaweza kujikuta unayapa mambo mengine kipaumbele kuliko elimu. Ukakosa muda wa kuzingatia masomo na kujiandaa na mitihani. Hili hupelekea wengi kufeli mitihani na kulazimika kurudia masomo hayo tena na tena. Hili huwachelewesha kuhitimu masomo na kupelekea wengine kukata tamaa na kuacha.

Kuepuka hilo, unapaswa kujipanga vizuri, kila unapoanza masomo, jua mambo yote unayopaswa kusomana jua mitihani ni kipindi gani na yapi yanaulizwa kwenye mitihani. Baada ya hapo tengeneza ratiba yako ya siku, ambayo inahusisha muda wa masomo wa kuwa darasani, muda wa kujisomea wewe mwenyewe na muda wa kufuatilia biashara zako.

Kumbuka hiyo ni kila siku, wengi husubiri mpaka mitihani ikaribie ndiyo wanaanza kujisomea, hilo linawafanya kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao.

Kwa hayo machache, nina imani unaweza kurudi shule na kufanya vizuri ili kuweza kufikia ndoto kubwa ya maisha yako. Usikubali yeyote awe sababu ya wewe kufikia ndoto ya maisha yako. Pia unapochagua safari hii, jua hakuna kurudi nyuma, iwe utakutana na magumu kiasi gani, unapaswa kuendelea na safari mpaka ufike kwenye ndoto yako.

Neno la mwisho; INAWEZEKANA, kama kweli utaweka juhudi kubwa na muda katika kufikia ndoto yako.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog