Hongera rafiki kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni siku bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kuba ili tuweze kupata matokeo bora sana. Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa kwa msingi huu.

Karibu kwenye makala hizi za ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufanikiwa. Huwa tunakuwa na mipango mizuri na mikubwa, lakini katika utekelezaji tumekuwa tunakutana na changamoto ambazo kwa wengine zimekuwa ndiyo mwisho kabisa wa ndoto hizo.

Leo tunakwenda kuangalia jinsi ya kuifanyia kazi ndoto yako hata kama unaona muda umekwenda. Kwa ile ndoto ambayo kweli inatoka ndani yako, huwa haina ukomo, hupaswi kuizika, hata kama umechelewa kuifanyia kazi. Zipo hatua ambazo mtu unaweza kuchukua na kuishi maisha ya ndoto yako.

Unashindwa

Kabla hatujaangalia kwa kina jinsi gani tunaweza kuishi ndoto zetu, kwanza tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili;

Nina hali ya hofu na kukata tamaa imepelekea kufanya vitu nje na ndoto yangu. Miaka tisa iliopita nilikua askari Magereza kwa kukosa uendelezaji wa kipaji changu na moyo ulivyokua unanisumbua niliacha kazi 2015, Japo nilikua askari ila moyoni ndoto ilikua inanitesa kwa nini sifanyi hicho kitu. Ndoto yangu ni kuwa mwanariadha wa mbio fupi ambaye hajawahi tokea. Ndoto hii ninayo tangu Mwaka 2002. Ila changamoto ya hofu/woga, kutokujitambua, kuahirisha, kukutana tamaa. Vimepelekea kubaki njia panda na roho mbili kunijia nishike kipaji changu japo nina miaka 35 ila naweza timiza ndoto hio? Au niachane nacho hakitonisaidia tena? Roho inaniuma najiona maono mkubwa katika kipaji hichi ila nimekwama. Sina msaada wa kimawazo nifanyeje Ili niendelee mbele. Ni hayo kaka. – Bilal R. M.

Kama alivyotuandikia Ndugu Bilal, wapo watu wengi ambao wamekuja kustuka baadaye kwenye maisha na kugundua mbio zote walizokuwa wanakimbia hazikuwa na maana.

Mara zote mchezo huwa unaanza hivi, mtu ni masikini, ametokea familia ambayo ni masikini na maisha ni magumu. Katika hali ya aina hiyo, fedha inakuwa ndiyo kipaumbele cha mtu huyo, kwa sababu bila fedha, shida alizonazo haziwezi kuondoka.

Hivyo anakuwa tayari kufanya lolote ili tu apate fedha, hapa mtu anaingia kwenye kazi au biashara yoyote anayoona inaweza kumpa fedha za kuweza kuendesha maisha yake. Anakazana sana kufanya kazi na fedha anazipata, maisha yanaanza kuwa bora.

Na hapo sasa ndipo ukweli unapoanza kuonekana, pamoja na kuwa na fedha mtu bado anakuwa anaona kuna kitu kinakosekana. Pamoja na kuwa na kazi au biashara inayomwingizia kipato, bado ndani yake kunakuwa na utupu ambao unamfanya atafute kitu cha kuujaza.

Hapa ndipo wengi hutafuta kitu cha kuwasumbua na kuwaondoa kwenye utupu huo. Wapo ambao huishia kwenye ulevi, kwa sababu tu hawapo tayari kuyakabili maisha yao. Na wapo ambao wanakuwa njia panda, je wafanyie kazi ndoto zao au wameshachelewa?

Hapa ndipo ndugu yetu Bilal amefikia, na mimi namwambia, usikubali kuzika ndoto yako, hata kama unaona umri umekwenda kiasi gani.

Nimekuwa nawaambia watu kitu kimoja, huwezi kujikimbia wewe mwenyewe. Yaani huwezi kabisa kuficha kile ambacho kipo ndani yako. Kwa sababu wewe utaendelea kuwa na wewe. unapokwenda kulala usiku, utajikumbusha kwamba hujaishi ndoto zako.

Hata kama utafanikiwa kiasi gani kwenye maeneo mengine ya maisha yako, kama hutafanyia kazi ndoto zako, mafanikio yako hayatakuwa kitu, tena yatakutesa zaidi.

Hivyo usikubali kabisa kuzika ndoto zako, kwa sababu hazipotei, zitaendelea kukuandama maisha yako yote.

SOMA; USHAURI; Mambo Ya Kuzingatia Kama Unataka Kurudi Shuleni Ili Kukamilisha Ndoto Zako.

Kuhusu umri, hakuna ukomo wa umri katika kufanya kile ambacho kweli mtu unakiamini. Tumekuwa tunaona watu wengi wakibadili maisha yao uzeeni kabisa. Wapo ambao wanaanza biashara wakiwa na miaka zaidi ya 60 na zinafanikiwa. Wapo ambao wanaanza elimu zao wakiwa na miaka mingi, na wanamaliza masomo na kufanya kile wanachotaka kufanya.

Hivyo usizuiwe na umri, kama kitu unakipenda kweli, ipo njia ya kukifanya, ambayo itakuwa ni utekelezaji wa ndoto zako.

Kwa mfano kwa Ndugu yetu Bilal ambaye ndoto yake ni kuwa Mwanariadha, wengi wanaweza kuwa na wasiwasi iwapo kwa umri wa miaka 35 mtu anaweza kuwa mwanariadha. Ukweli ni kwamba inawezekana, tunaona wanariadha wengi wakifanya riadha wakiwa na umri mkubwa. Kikubwa ni kujifunza njia bora ya kukamilisha ndoto yako kwa umri wowote mtu alionao. Ufanyaji wa mazoezi na maandalizi yanapaswa kuwa tofauti kwa mtu mwenye umri mkubwa.

Kama umri utashindikana kabisa, labda kiafya ikawa haiwezekani kuwa mwanariadha unayetaka kuwa, bado huo siyo mwisho wa ndoto yako. Unaweza kujihusisha na riadha kwa ngazi tofauti. Unaweza kujifunza na kuwa mwalimu wa riadha, na hivyo kuwasaidia wengine kuwa wanariadha bora kabisa. Kwa njia hii utakuwa umeiishi ndoto ya maisha yako kupitia wengine, na pia itakuridhisha zaidi.

Unaweza pia kuwa mchambuzi wa mambo yanayohusu riadha, kuwa mwandishi kuhusu riadha na kuwapa watu wengine maarifa muhimu kuhusu riadha.

Kwa vyovyote vile, yapo mambo mengi unayoweza kufanya kwenye ndoto yoyote uliyonayo, hata kama huwezi kuifanya ndoto ile moja kwa moja. Muhimu ni wewe kuangalia pale ulipo kipi unachoweza kufanya.

Kitu kikubwa cha kuepuka ni kuizika ndoto yako, itakutesa maisha yako yote. Hivyo hata kama una kazi au biashara nyingine inayokuingizia kipato, tenga muda wa kufanyia kazi ndoto yako hata kama ni kwa hatua ndogo.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog