Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?

Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu CHAGUO RAHISI NI CHAGUO BAYA…

Kwenye kila jambo tunalofanya kwenye maisha yetu, au hali tunazokutana nazo, huwa tunakuwa na machaguo mbalimbali. Huwa tunakuwa na hatua tofauti za kuchukua.

Katika machaguo hayo, yapo ambayo ni rahisi na yapo ambayo ni magumu.

Kwa kuwa watu huwa hatupendi kujisumbua, huwa tunakimbilia kuchukua chaguo ambalo ni rahisi. Hapo ndipo tunapofanya makosa makubwa.

Chaguo rahisi mara nyingi huwa ni chaguo baya.

Chaguo rahisi huwa linatengeneza matatizo zaidi baadaye, au kutufanya tusione matatizo na siyo kutatua matatizo tuliyonayo.

Kwa mfano, mtu anapokuwa na changamoto nyingi zinazopelekea kupata msongo wa mawazo, njia rahisi ni kutumia kilevi, kuwalaumu wengine, na hata kukataa majukumu yake yanayopelekea changamoto hizo. Chaguo gumu ni kukubali changamoto hizo na kuamua kuzifanyia kazi, kutatua ili kuondokana nazo.

Wengi sana hukimbilia chaguo la kwanza ambalo ni rahisi, na wanashangaa kwa nini matatizo na changamoto haviishi.

Kila hatua unayochukua kwenye maisha yako, jiulize kwanza je hii ni hatua rahisi au ngumu kuchukua. Angalia hatua zote ambazo ungeweza kuchukua kwenye hali yoyote, na kama hatua unayochukua ni rahisi, jua unasogeza tatizo au changamoto mbele, huitatui.

Machaguo rahisi na hata njia rahisi siyo salama katika kufika kule tunakotaka, kwenye maisha ya mafanikio. Achana nazo.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz