Moja ya kanuni kubwa ya kimafanikio ambayo unatakiwa kuanza kuitumia ni KUKATAA KUTOA SABABU YOYOTE. Kama kuna kitu unakifanya, kifanye. Kama kuna kitu umeshindwa kukifanya huna haja ya kuendelea kutoa sababu kwa nini umeshindwa. Acha kutumia ubongo wako hovyo kwa kutoa sababu. Uelewe sababu unazozitoa hata ziwe nzuri vipi haziwezi kukusaidia. Unataka kufanikiwa, usiendelee tena kutoa sababu kwenye maisha yako, NO MORE EXCUSE IN YOUR LIFE.

Watu wanaoshindwa ni watu wa kutoa sababu kila siku. Watu wa mafanikio ni watu wa kuchukua hatua. Jiulize au waangalie wale wote wanaotoa sababu kama wewe, kuna mafanikio ambayo wamepata? Ukiangalia, hakuna mafanikio waliyopata. Hiyo ni ishara tosha kama unaendelea kutoa sababu pia ni ngumu kuweza kufanikiwa.

Kitu kimoja ambacho karibu vitabu vyote vya mafanikio na watu wote wa mafanikio wanakubaliana nacho, ni umuhimu wa kuwa nidhamu binafsi katika kuelekea mafanikio. Nidhamu binafsi inaelezwa kama ndio nguzo ya kufikia mafanikio makubwa.

Kufanikisha makubwa katika maisha sio swala la muujiza, bali inahitaji kwanza na wewe uwe wa tofauti. Huwezi kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kama wewe unaendelea ndani yako kubaki vile vile. Yanahitajika mabadiliko makubwa sana ndani yako ili ufanikiwe kwa viwango vya juu.

Hata uwe na siri nyingi vipi za mafanikio, lakini siri ya kwanza na ya muhimu katika kufikia mafanikio ni NIDHAMU BINAFSI. Nidhamu binafsi inatufundisha kufanya kile tunachotakiwa kufanya bila kujali kama unajisikia kufanya au haujisikii, lakini kwa sababu ya nidhamu binafsi unafanya.

SOMA; Mambo Muhimu Ya Kujifunza Kuhusu Nidhamu Binafsi Na Mafanikio.

Anguko kubwa la maisha ya wengi linatokana na wao kukosa nidhamu binafsi. Unapokosa nidhamu binafsi unashindwa kutawala maisha yako, unashindwa kujizuia, unashindwa kujikana na hata pia unashindwa kuvumilia ili kupata faida za muda mrefu.

Huna budi kujifunza juu ya nidhamu binafsi. Hata kama ugumu upo, lakini unatakiwa kujifunza. Kwanza ukumbuke, kila kitu kilianza kuwa kigumu kabla hakijawa rahisi. Hakuna ambacho rahisi hakikuanza kwa ugumu, lazima kilianza kwa ugumu tena sana.

Tafsiri rahisi ya mafanikio ni kufanya vile vitu unavyovipenda maishani mwako. Tafsiri ya mafanikio haipo kwa mtu mwingine. Jiulize, nini unakipenda, kifanye kitu hicho kwa uhakika hadi kikufikishe kwenye lengo.

Sababu kubwa mbili zinazopelekea wengi kushindwa katika maisha yao ni kukosa nidhamu na kutoa sababu sana/visingizio.                                                      

Mbali na nidhamu binafsi, siri nyingine muhimu katika mafanikio ni kujifunza kwa waliofanikiwa tayari. Jukumu lako kubwa ni kutakiwa kukaa chini na kujifunza mambo muhimu kutoka kwa ambao tayari wameshafanikiwa kutokana na yale unayoyataka kuyafanya. Soma vitabu vyao, hudhuria warsha na semina zao na wewe utajikuta ukifikia mafanikio hayo, ikiwa utafanya hayo kwa mwendelezo mkubwa.

Ni wako rafiki katika mafanikio,

Imani Ngwangwalu,

Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,

Tovuti; http://www.amkamtanzania.com

Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com