Kama umekuwa unasikia kuhusu uwekezaji kwa hapa Tanzania, basi utakuwa umesikia kuhusu soko la hisa la dar es salaam kwa kiingereza Dar es salaam Stock Exchange (DSE).

Huenda umekuwa unasikia na kuona hilo kwenye taarifa mbalimbali za habari.

Swali ni je unaposikia soko la hisa ni mawazo gani yanakujia kwenye akili yako?

Kwa wengi ambao wamekuwa wananiuliza kuhusu hili, wamekuwa wakifikiri soko la hisa ni eneo ambalo kila mtu anaweza kwenda na kununua hisa. Na hiyo siyo sahihi.

Katika makala haya ya UWEKEZAJI LEO nakwenda kukushirikisha kuhusu soko la hisa la Dar, jinsi linavyofanya kazi na wewe unawezaje kunufaika nalo.

Kwanza tuanze na hisa;

Hisa ni aina ya uwekezaji ambapo mtu anapata nafasi ya kuwa sehemu ya wamiliki wa kampuni au biashara. Kwa kununua hisa za kampuni fulani, maana yake umechangia kwenye mtaji wa kampuni ile.

Unaponunua hisa, fedha yako inatumika kwenye uzalishaji na shughuli mbalimbali za kampuni, lakini wewe huhusiki moja kwa moja kwenye kuendesha shughuli hizo. Iwapo kampuni itapata faida basi wenye hisa pia wanapata faida. Kampuni ikipata hasara wenye hisa pia wanapata hasara.

dse-dar-es-salaam-stock-exchange-tanzania

Soko la hisa.

Soko la hisa, kwa lugha rahisi tunaweza kusema ni sehemu ambayo watu wanakutaka katika kuuza na kununua amana mbalimbali za uwekezaji.

Soko la hisa linatoa fursa kwa makampuni kuongeza mtaji kwa kuuza hisa zake kwa watu. Na pia linatoa fursa kwa mtu mmoja mmoja na hata kampuni au taasisi kuwa sehemu ya umiliki wa kampuni nyingine kwa kununua hisa.

Soko la hisa ndiyo mhimili mkuu wa uwekezaji wa amana kwenye kila nchi. Kila nchi ina soko lake la hisa, na baadhi ya nchi zina soko zaidi ya moja.

Soko la hisa la Dar es salaam.

Hili ndiyo soko la hisa lenye mamlaka ya kudhibiti uuzaji na ununuaji wa amana za makampuni na taasisi mbalimbali.

Kupitia soko la hisa la Dar, kampuni inaweza kujiandikisha kuuza hisa zake, na pia wananchi wanaweza kununua hisa za makampuni mbalimbali.

Je unaendaje kununua hisa DSE?

Huwezi kwenda moja kwa moja kwenye soko la hisa na kununua hisa. Badala yake unapitia kwa mawakala wa soko la hisa, ambao kwa lugha ya uwekezaji wanaitwa MADALALI WA SOKO LA HISA.

Haya ni makampuni yanayotambuliwa kisheria ambayo yanakuwezesha wewe kununua au kuuza hisa zako kwenye soko la hisa.

Unanunuaje au kuuzaje hisa?

Iwapo unataka kununua hisa, kwanza lazima ujue kampuni ambayo unataka kununa hisa zake, au kuomba ushauri wa kampuni ipi nzuri kununua hisa zake, unaenda kwenye ofisi za madalali hawa wa soko la hisa, huko utajaza fomu maalumu ya ununuaji wa hisa, utaweka fedha kwenye akaunti yao.

Baada ya kukamilisha hilo, wao watashiriki kwenye soko la hisa na kununua kulingana na uhitaji wako na upatikanaji wa hisa husika. Wakati mwingine unaweza kupata kwa haraka, huku wakati mwingine ukihitaji kusubiri.

Baada ya hisa kununuliwa, unachapishiwa cheti kinachoonesha kwamba wewe ni mmiliki wa hisa za kampuni fulani, cheti hichi unakuwa nacho wewe mwanahisa na ndiyo utakitumia wakati wa kuuza.

Utaratibu wa kuuza hisa ni kama huo wa kununua, unapitia kwa dalali na kujaza fomu ya kuuza, kisha yeye anaziweka sokoni, zinaponunuliwa fedha unawekewa kwenye akaunti yako ya benki.

Maswali unayoweza kujiuliza na majibu yake;

Je ni makampuni gani yanapatikana kwenye soko la hisa la Dar es salaam? Jibu, bonyeza maandishi haya kuna orodha ya makampuni yote.

Je madalali wa soko la hisa ni kina nani na naweza kuwapata wapi? Jibu, bonyeza maandishi haya na utapata orodha ya madalali na mawasiliano yao.

Tutaendelea kujifunza kuhusu uwekezaji kwenye makala hizi za UWEKEZAJI LEO, lengo ni kila mmoja wetu kuwa mwekezaji bora na anayenufaika kupitia uwekezaji.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog