Wakati unapoanza biashara yoyote, huwa unakuwa na mawazo yako juu ya biashara hiyo. Huwa unakuwa na mipango mikubwa juu ya biashara yako na wateja unaowalenga pia.

Lakini unapoingia kwenye biashara hasa, mambo huwa tofauti na ulivyotegemea. Wakati mwingine kitu ulichofikiri wateja wanakitaka kweli kinakuwa siyo kitu chenyewe.

IMG-20170406-WA0003

Hili linakufanya ubadili biashara yako kadiri inavyokwenda, kwa namna ambavyo unawasoma wateja wako.

Lakini kuna hali ambazo hazipaswi kukufanya ubadili biashara yako. Anaweza kuja mteja, ambaye anahitaji kitu tofauti kabisa na biashara unayofanya wewe, lakini ukaona unaweza kukifanya, ila hakiendani na biashara yako.

Hapa wengi huwa wazito kusema HAPANA au HAWAWEZI, hivyo huwapa wateja kile wanachotaka, na baada ya hapo hubadili biashara kujumuisha kile ambacho mteja mmoja amekitaka. Hapa ndipo wengi huanza kuvuruga biashara zao, kwa sababu anaweza kuja mteja mwingine tena na hitaji lingine, naye wakamkubalia.

SOMA; Tabia Za Wajasiriamali Wakubwa Ambazo Huwezi Kuzikuta Kwa Watu Wengi.

Baada ya muda mtu anajikuta anafanya vitu vingi na ambavyo havina mahusiano ya karibu. Anajikuta anaichukia biashara na kuona ni ngumu kwa sababu mambo mengi yanamhitaji yeye afanye.

Hivyo unapaswa kuwa makini sana na biashara unayofanya, jiwekee mipaka ambayo hata kama unabadilika, basi hutaivuka. Usikubali maoni au mahitaji ya mteja mmoja yakakupelekea wewe kubadili kabisa biashara unayofanya.

Usiogope kusema HAPANA au SIWEZI kwa kuhofia kuwapoteza wateja. Badala yake waeleze nini watapata kwako na ukiweza washauri sehemu bora kabisa ya kupata kile ambacho wanakitaka.

Wakienda huko watakipata kwa ubora, na hawatakusahau wewe, watakapokuwa na hitaji linaloendana na biashara yako, watakuja kwenye biashara yako.

Mabadiliko ya biashara ni muhimu, lakini kama mabadiliko yanabadili kabisa biashara yako, yasiwe yanatoka kwa mteja mmoja.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog