Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni siku bora na ya kipekee sana kwetu ambapo tunakwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa sana.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu SIYO MARA MOJA….

Katika kila jambo muhimu kwenye maisha yetu, huwa tunalifanya siyo mara moja.

Huwezi kula mara moja ukasema basi umemalizana na mambo ya kula na maisha yako yataendelea kuwa vizuri kiafya.

Au ukasema ukishaoga mara moja basi utakuwa msafi kila siku.

Unahitaji kula na kuoga kila siku ili afya yako iwe nzuri na uwe kwenye hali ya usafi. Ni KILA SIKU.

Lakini linapokuja swala la kazi, mafanikio na hata hamasa, watu wanatafuta kitu cha kufanya mara moja halafu wapate matokeo ya kudumu.

Watu wanatafuta hamasa moja ambayo itadumu nao kwa muda mrefu,

Au fursa moja ambayo watafanya kitu kimoja na hapo watapata kila wanachotaka.

Huku ni kujidanganya, na kumepelekea wengi kukosa kile wanachotaka.

Huwezi kufanya chochote mara moja na kusubiri matokeo makubwa, lazima uendelee kufanya tena na tena na kwa muda mrefu.

Matokeo madogo madogo yanajikusanya na kuwa matokeo makubwa.

Unapofikiria kuhusu mafanikio, jiulize kitu gani upo tayari kufanya kila siku bila ya kuchoka.

Linapokuja swala la kujifunza, linapaswa kuwa zoezi la kila siku.

Hakuna kitu unachoweza kufanya mara moja pekee kikaleta matokeo yote unayotaka.

Unahitaji kurudia kufanya tena na tena, kila siku na kila mara.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz