Moja ya mjadala mkubwa kwenye biashara, hasa biashara ndogo ni iwapo mtu unaweza kuvutia wateja zaidi kwa kuweka punguzo la bei, au kuuza bei rahisi kuliko wengine.
Na mara nyingi majibu ni ndiyo ndani ya muda mfupi, utavutia wateja ndani ya muda mfupi, lakini iwapo na wengine nao watapunguza bei, basi mtaendelea kugawana wateja.
Lakini pia bei inapokuwa chini, ndivyo faida inavyokuwa ndogo na ndivyo uendeshaji wa biashara unavyokuwa mgumu. Huduma zinakuwa mbovu na wateja wengi hawapati kile walitegemea kupata.

Dawa pekee ya kuepuka kuingia kwenye ushindani wa kupunguza bei, ni kuwa na bidhaa bora kabisa, ambayo mteja hawezi kuipata sehemu nyingine yoyote. Hapo mteja anakuwa anaithamini sana ile bidhaa, hasa inapokuwa ndiyo tegemeo pekee kwenye kutatua matatizo na changamoto zake.
Lakini wafanyabiashara wengi hawana starehe hii ya kuchagua ubora wa bidhaa, kwa sababu wao wananunua jumla na kuuza rejareja. Hapo wengi huona hawana namna bali kupambana kupitia bei.
Lakini yapo ambayo mtu anaweza kufanya, na akaweza kuwa na wateja waaminifu kwenye biashara bila ya kukimbilia kupunguza bei. Baadhi ya hayo ni;
- Kuhakikisha unauza bidhaa ambazo ni bora kabisa, hata kama unanunua jumla, basi nunua bidhaa za kampuni ambazo ni bora kabisa, ambazo zinaaminika. Hata kama gharama itakuwa juu kidogo, utapata wateja ambao wanajali ubora wanaopata.
- Toa huduma bora sana. Hata kama bidhaa unapata kwa wengine, lakini huduma kwa wateja wako unatoa wewe. hapa hakikisha wateja wako wanapata huduma bora sana, huduma ambayo hawawezi kuipata kwingine, hili litawavutia kuja kwako zaidi.
- Ondoa changamoto ndogondogo zisizo za lazima kwa wateja. Vitu kama kusubiri kwa muda mrefu, kupewa tofauti na alichoagiza na hata kuambiwa hakuna chenchi, huwa vinawakera wateja. Wewe kama mfanyabiashara, hakikisha vitu hivi vidogo vidogo haviwi kero kwa wateja wako.
Kwa vyovyote vile, kama kusudi lako ni kujenga biashara ambayo itadumu kwa muda mrefu na siyo tu kupata fedha za haraka, kupunguza bei siyo njia bora ya kukuza wateja wako. Kazana kuongeza thamani zaidi, ambayo wateja hawaipati sehemu nyingine bali kwenye biashara yako. Na vipo vitu vingi vidogo vidogo ambavyo ukifanya vitaongeza sana thamani kwenye biashara yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog