Kwenye makala iliyopita ya UWEKEZAJI LEO, tuliona kwamba amana kuu mbili zinazopatikana kwenye soko la hisa la Dar ni hisa na hatifungani.
Watu wengi wamekuwa wakisikia hisa mara kwa mara, lakini siyo hatifungani. Na hii ni kwa sababu zipo kampuni nyingi zinazouza hisa zake kuliko zinazouza hatifungani.
Katika makala haya ya leo, nakwenda kukushirikisha msingi mkuu wa hisa na hatifungani, ili kuelewa tofauti zake na jinsi ya kuzitumia katika uwekezaji.
Yapo mengi sana tunaweza kujifunza kuhusu tofauti za hisa na hatifungani, lakini hapa nakwenda kukupa msingi mkuu wa tofauti hizo, baada ya hapo utaelewa kwa kina kuhusu amana hizi mbili.

Hisa.
Kama ambavyo unajua mpaka sasa, hisa ni aina ya uwekezaji ambapo mtu anachangia mtaji kwenye biashara, kwa kununua sehemu ya umiliki wa biashara. Unaponunua hisa, maana yake umechagua kuwa sehemu ya wamiliki wa biashara. Hivyo chochote kinachotokea kwenye biashara, kinahusisha mtaji wako ulioweka.
Kwa mfano kama biashara itapata faida, basi mwanahisa unapata faida kwa njia ya gawio na hata kupanda thamani kwa hisa zako. Na kama biashara itapata hasara, basi hutapata gawio na huenda thamani ha hisa ikashuka na ukawa umepoteza mtaji wako.
Kitu kizuri kwenye hisa ni kwamba, faida unayoweza kupata ni kubwa kulingana na uchumi unavyokwenda.
Lakini pia unaweza kupata hasara kubwa iwapo mambo hayatakwenda vizuri.
Hatifungani.
Hii ni aina ya uwekezaji ambapo mtu unaikopesha kampuni au taasisi fedha, inakwenda kuzifanyia kazi halafu inakulipa baada ya muda fulani. Kwenye uwekezaji huu, unaponunua hatifungani, unaambiwa ni riba kiasi gani utapewa. Hivyo mtaji ulioweka utatumika kwa kipindi ulichoweka, utapewa riba na mwisho wa hatifungani unarudishiwa mtaji wako wote ulioweka.
Kwa haraka unaweza kuona namna gani uwekezaji huu ni salama, kwa sababu hata uchumi uende vibaya kiasi gani, mtaji wako kwa asilimia kubwa upo salama, na riba yako itabidi upewe. Na hiyo ni kweli, ukilinganisha hisa na hatifungani, hatifungani zina usalama mkubwa wa mtaji ambao mtu unawekeza.
Changamoto ya hatifungani ni kwamba riba huwa ni kidogo hivyo mapato kutoka kwenye uwekezaji huo kuwa kidogo sana.
Kwa mfano, kuna kampuni A ambayo inauza hisa na hatifungani kwa pamoja. Mtaji wa kampuni ni milioni mia moja. Inahitaji kupata milioni 10 za kufanyia kazi kwa mwaka mmoja. Ikauza hisa na hatifungani ili kupata fedha hiyo. Wewe ukanunua hisa za milioni tano, na mwenzako akanunua hatifungani ya milioni 5, kwa ahadi ya kupata asilimia 7 kwa mwaka.
Mwisho wa mwaka, kampuni imepata faida ya asilimia 10 baada ya kutoa gharama zake zote za uendeshaji. Ukigawa faida hiyo kulingana na hisa, wewe utapata shilingi laki tano kwa milioni t uliyoweka. Wakati mwenzako atapata shilingi laki tatu na nusu kwa milioni tano aliyoweka.
Iwapo mwisho wa mwaka umefika, kampuni imepata hasara na inahitaji kufilisiwa, mali zake zitauzwa na kati yenu wawili, mwenzako ndiyo atapewa kipaumbele cha kwanza kwenye kulipwa fedha yake na riba yake. Wewe utapata kile kitakachobakia, kama hata kitabaki kitu.
Nina imani umepata kitu hapo kwenye tofauti ya msingi ya Hisa na Hatifungani, kama una swali lolote uliza hapo chini kwenye maoni na nitakujibu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
Asante sana Kocha kwa elimu hii, naomba kujua juu ya ongezeko la thamani ya mtaji kwenye Hisa na Hatifungani ipo sawa? Pia kuna mfuko nimesoma kwenye uwekezaji wa Hatifungani UTT kuwa wanatoa Hatifungani kwa malipo ya kila mwezi na yenye ongezeko la thamani, imekaaje hii? Naomba kueleweshwa hapo. Asante.
LikeLike
Hatifungani za kawaida hazina ongezeko la thamani, unachopata ni ile riba inayotolewa na hatifungani hiyo, lakini mwisho msingi ulioweka unakuwa ni ule ule.
Hisa huwa zina ongezeko la thamani kulingana na ufanisi wa kampuni husika, kama inatengeneza faida na kufanya vizuri mtaji wake unakua na hapo thamani ya hisa inaongezeka. Wakati mwingine pia soko linaweza kufanya thamani ya hisa kuongezeka, pale watu wengi wanapohitaji hisa za kampuni fulani, basi bei yake hupanda na hapo kunakuwa na ongezeko la thamani.
Mfuko wa hatifungani wa UTT unatofautiana na hatifungani za kawaida, kwa sababu hatifungani za UTT zipo kwenye soko la wazi, ambapo mtu anaweza kununua na kuuza wakati wowote. Hivyo thamani yake inategemea na hali ya soko, ndiyo maana pamoja na malipo ya kila mwezi, unaweza kunufaika pia na ongezeko la thamani kama bei ya kipande itaongezeka pale soko linapokuwa vizuri. Hatifungani za UTT zinauza kwa vipande, hivyo kama umenunua kipande leo kwa tsh 100, halafu mwaka kesho kikawa kimefikia bei ta tsh 120, kuna ongezeko la thamani ya tsh 20 kwa kila kipande unachomiliki.
LikeLike