Kwenye makala iliyopita ya UWEKEZAJI LEO, tuliona kwamba amana kuu mbili zinazopatikana kwenye soko la hisa la Dar ni hisa na hatifungani.

Watu wengi wamekuwa wakisikia hisa mara kwa mara, lakini siyo hatifungani. Na hii ni kwa sababu zipo kampuni nyingi zinazouza hisa zake kuliko zinazouza hatifungani.

Katika makala haya ya leo, nakwenda kukushirikisha msingi mkuu wa hisa na hatifungani, ili kuelewa tofauti zake na jinsi ya kuzitumia katika uwekezaji.

Yapo mengi sana tunaweza kujifunza kuhusu tofauti za hisa na hatifungani, lakini hapa nakwenda kukupa msingi mkuu wa tofauti hizo, baada ya hapo utaelewa kwa kina kuhusu amana hizi mbili.

hisa na hatifungani

Hisa.

Kama ambavyo unajua mpaka sasa, hisa ni aina ya uwekezaji ambapo mtu anachangia mtaji kwenye biashara, kwa kununua sehemu ya umiliki wa biashara. Unaponunua hisa, maana yake umechagua kuwa sehemu ya wamiliki wa biashara. Hivyo chochote kinachotokea kwenye biashara, kinahusisha mtaji wako ulioweka.

Kwa mfano kama biashara itapata faida, basi mwanahisa unapata faida kwa njia ya gawio na hata kupanda thamani kwa hisa zako. Na kama biashara itapata hasara, basi hutapata gawio na huenda thamani ha hisa ikashuka na ukawa umepoteza mtaji wako.

Kitu kizuri kwenye hisa ni kwamba, faida unayoweza kupata ni kubwa kulingana na uchumi unavyokwenda.

Lakini pia unaweza kupata hasara kubwa iwapo mambo hayatakwenda vizuri.

Hatifungani.

Hii ni aina ya uwekezaji ambapo mtu unaikopesha kampuni au taasisi fedha, inakwenda kuzifanyia kazi halafu inakulipa baada ya muda fulani. Kwenye uwekezaji huu, unaponunua hatifungani, unaambiwa ni riba kiasi gani utapewa. Hivyo mtaji ulioweka utatumika kwa kipindi ulichoweka, utapewa riba na mwisho wa hatifungani unarudishiwa mtaji wako wote ulioweka.

Kwa haraka unaweza kuona namna gani uwekezaji huu ni salama, kwa sababu hata uchumi uende vibaya kiasi gani, mtaji wako kwa asilimia kubwa upo salama, na riba yako itabidi upewe. Na hiyo ni kweli, ukilinganisha hisa na hatifungani, hatifungani zina usalama mkubwa wa mtaji ambao mtu unawekeza.

Changamoto ya hatifungani ni kwamba riba huwa ni kidogo hivyo mapato kutoka kwenye uwekezaji huo kuwa kidogo sana.

Kwa mfano, kuna kampuni A ambayo inauza hisa na hatifungani kwa pamoja. Mtaji wa kampuni ni milioni mia moja. Inahitaji kupata milioni 10 za kufanyia kazi kwa mwaka mmoja. Ikauza hisa na hatifungani ili kupata fedha hiyo. Wewe ukanunua hisa za milioni tano, na mwenzako akanunua hatifungani ya milioni 5, kwa ahadi ya kupata asilimia 7 kwa mwaka.

Mwisho wa mwaka, kampuni imepata faida ya asilimia 10 baada ya kutoa gharama zake zote za uendeshaji. Ukigawa faida hiyo kulingana na hisa, wewe utapata shilingi laki tano kwa milioni t uliyoweka. Wakati mwenzako atapata shilingi laki tatu na nusu kwa milioni tano aliyoweka.

Iwapo mwisho wa mwaka umefika, kampuni imepata hasara na inahitaji kufilisiwa, mali zake zitauzwa na kati yenu wawili, mwenzako ndiyo atapewa kipaumbele cha kwanza kwenye kulipwa fedha yake na riba yake. Wewe utapata kile kitakachobakia, kama hata kitabaki kitu.

Nina imani umepata kitu hapo kwenye tofauti ya msingi ya Hisa na Hatifungani, kama una swali lolote uliza hapo chini kwenye maoni na nitakujibu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog