Hii ni dhana ambayo itakusaidia sana kubadili mtazamo wako kibiashara, hasa pale unapokutana na mteja wako.
Japokuwa upo kwenye biashara kuuza bidhaa na huduma unazotoa, kumbuka kwamba mteja haji kwako kwa sababu wewe unauza. Bali mteja anakuja kwako kwa sababu ana shida au changamoto, na ana amini ya kwamba wewe unaweza kumsaidia kuitatua.
Hivyo unachopaswa kufanya pale unapokuwa na mteja wako, usikazane kumuuzia, bali mshawishi kununua. Fanya mteja aone anakwenda kuchukua hatua muhimu ya kuboresha maisha yake kupitia kile ambacho ananunua kwako.

Hata unapoandaa tangazo au maelezo ya biashara yako, andaa kwa njia ambayo inamshawishi mteja kununua, na siyo kwa njia ya wewe kusukuma au kuuza.
Usimwambie mteja kwa nini wewe ni bora na umewashinda wengine, bali mwambie kwa nini yeye anapaswa kununua kile ambacho unauza.
Ni mabadiliko madogo kimtazamo, lakini yana matokeo tofauti kabisa kwenye biashara yako.
Mteja anapogundua kwamba anakazaniwa kununua, anapata wasiwasi kwa nini mkazo uwekwe kiasi hicho. Lakini anapokuwa anapata msukumo kutoka ndani yake, wa kununua, wa kuona kuna kitu anakosa, anafanya maamuzi ambayo ataendelea kuyafurahia.
SOMA; BIASHARA LEO; Cross-Selling Na Up-Selling, Mbinu Mbili Za Kuongeza Mauzo Bila Kuongeza Wateja.
Nimekukumbusha hili rafiki kwa sababu wakati mwingine tunapoweka mikakati yetu ya kibiashara tunasahau kwamba wateja ni watu, ambao nao wana hisia na mahitaji yao. Tukikumbuka hilo na kutumia hisia na mahitaji hayo, tunaweza kuwasaidia wateja kutatua changamoto zao.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog