Habari za leo rafiki yangu?

Ni imani yangu kwamba unaendelea vizuri, ukiweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa. Najua ya kwamba unajua hatua unazochukua leo ndiyo zinatengeneza maisha bora ya kesho, hivyo kama unataka maisha mazuri kesho, huna budi kuchukua hatua kubwa leo.

Leo nina ujumbe mfupi sana kwako, ambao ni muhimu sana wakati unaendelea na safari yako ya mafanikio. Kwa hakika ni mambo mawili nakwenda kukushirikisha, ndani ya ujumbe huu mfupi.

Jambo la kwanza ni hujachelewa.

Upo usemi kwamba, wakati bora kabisa wa kupanda mti ulikuwa miaka 20 iliyopita. Kama ungepanda mti miaka 20 iliyopita leo ungekuwa unafaidi matunda na kivuli.

Lakini je kama hukupanda mti miaka hiyo 20 iliyopita ndiyo umeshapoteza na hakuna tena matumaini kwako?

Jibu ni hapana, sehemu ya pili ya usemi huo inamalizia kwamba wakati mwingine bora wa kupanda mti ni leo. Hivyo kuna matumaini makubwa hapo, kama ulichelewa kupanda mti miaka 20 iliyopita, bado unayo nafasi ya kupanda mti leo, na miaka ijayo ukaweza kufaidi matunda na kivuli.

Nakupa ujumbe huu kwa sababu watu wengi wamekuwa wakiniandikia na kusema ningejua haya unayotufundisha leo miaka 20 au 10 iliyopita, leo ningekuwa mbali sana.

Nami nawaambia ni kweli, lakini je miaka 10 mpaka 20 ijayo unataka kuwa wapi? Na hatua gani unazokwenda kuchukua leo, kiasi kwamba miaka 10 mpaka 20 ijayo utaangalia nyuma na kushukuru hatua hii uliyochukua?

Unaona rafiki yangu, , watu watakuambia wamechelewa, halafu hawatachukua hatua yoyote, wataendelea na maisha yao waliyoyazoea, halafu siku zijazo watakuja kujutia tena na kusema ningejua…

Hivyo rafiki yangu, hakuna jambo lolote ambalo unachelewa hapa duniani, kama ulikuwa hujui, wakati wako wa kujua ulikuwa haujafika. Ila ukishajua halafu usifanye kitu, hapo sasa umechagua wewe mwenyewe kujichelewesha.

SOMA; Jambo La Muhimu Ambalo Hujachelewa Kulifanya Kwenye Maisha Yako.

Mambo gani unaweza kuanza leo na miaka 10 mpaka 20 ijayo ukavuna matunda yake?

Yapo mengi, hapa nitaje machache;

  1. Anza kujisomea vitabu kila siku, na fanyia kazi yale ambayo unajifunza.
  2. Anza kuwekeza, hata kama ni kiasi kidogo cha fedha, fanya hivyo kila siku, au kila wiki au kila mwezi, miaka kumi ijayo, utakuwa mbali sana.
  3. Anza biashara leo, anza na mteja mmoja, anzia popote ulipo, kisha endelea kukua.
  4. Anza kuweka ubora kwenye kila unachofanya, nenda hatua ya ziada kuliko wengine wanavyofanya.

Jambo la pili; huwezi kufanya kila kitu.

Jambo la pili, ambalo ni kama mwendelezo wa jambo la kwanza ni kwamba huwezi kufanya kila kitu.

Watu wanapogundua kwamba wamechelewa, basi wanahamaki, na kuanza kukazana kufanya kila kitu, wakiamini hilo litawasaidia kufika haraka. Hivyo basi wanataka wasome vitabu vingi kwa wakati mmoja, wawe na biashara nyingi, wawe na uwekezaji mkubwa na wajihusishe na kila kinachopita mbele yao.

Wakisikia chochote ni fursa au kinalipa sana basi hawakubali kiwapite. Na hili ndiyo linawapoteza wengi zaidi.

Hii inanikumbusha hadithi moja, ambapo kijana mmoja alienda kwa mzee na kumwomba ushauri kwamba anataka kuwa mtu mtulivu, mwenye amani na anayeweza kudhibiti mawazo yake. Akamuuliza itamchukua muda mrefu kiasi gani, mzee akamjibu miaka kumi. Kijana akamwambia, nipo tayari kufanya kazi usiku na mchana kufikia hilo, je itanichukua muda kiasi gani? Mzee akamjibu, miaka 20.

Unaona hapo, kadiri unavyokazana kulazimisha na kutaka kufanya kila kitu, ndivyo unavyozidi kupoteza muda mwingi zaidi.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Stop Sabotaging Your Career (Acha Kuihujumu Kazi Yako Wewe Mwenyewe).

Chagua maeneo machache ambayo unaweza kuweka akili yako, nguvu zako na imani yako yote, halafu fanyia kazi hayo, sahau kabisa kuhusu kelele nyingine zozote, acha kukimbizana na fursa zinazoibuka kila siku, na jipe muda, miaka 10 mpaka 20 ijayo, hutakuwa hapo ulipo sasa. Lakini, na nirudie kwa herufi kubwa LAKINI ni kama utachagua mambo machache na kuchukua hatua leo, kukomaa nayo mpaka upate matokeo unayotaka.

Hayo mawili yanatosha kwa leo rafiki, msisitizo wangu kwako ni kuchukua hatua, la sivyo haya yote yamekupotezea muda wako.

Vitu muhimu napenda kukukumbusha hapa;

  1. Kama umekuwa unapenda kusoma vitabu lakini unakosa muda, nimeandaa programu ambayo itakuwa nzuri sana kwako, unaweza kupata maelezo yake hapa; amkamtanzania.com/kurasa
  2. kama hujasoma kitabu cha MIMI NI MSHINDI, kuna mambo makubwa unayakosa, unapaswa kukipata na kuanza kukisoma mara moja. Upatikanaji wake ni kama inavyoonekana kwenye picha hapo chini.

MIMI NI MSHINDI

3. Mwisho, oktoba mwaka huu tuna semina ya kukutana moja kwa moja kwa wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, ili kushiriki semina hii unapaswa kudhibitisha kabla wiki hii haijaisha, kama bado hujadhibitisha, tuwasiliane kwa wasap 0717 396 253.

Uwe na siku njema sana ya leo rafiki yangu,

NIDHAMU, UADILIFU, KUJITUMA.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog