Watu wengi wamekuwa wakiona uwekezaji kwenye ununuzi wa hisa na amana nyingine kama aina ngumu ya uwekezaji, ambayo inaweza kufanywa na watu wenye fedha nyingi na wenye elimu kubwa.
Yote hayo ni uongo, kila mtu anaweza kuwekeza kwenye hisa, hata mwenye kipato kidogo na asiye na elimu kubwa.
Uwekezaji kwenye hisa hauna tofauti na mtu unapokwenda kununua shamba, kiwanja au nyumba.
Kwanza lazima ujue kile unachotaka, uwe na fedha na ujue unakipata wapi. Tukichukua mfano wa kiwanja, unaponunua unaweza kukaa nacho, usubiri bei ipande ndiyo uje uuze kwa bei ya juu. Au unaweza kununua leo, baada ya siku chache ukaona bei zimepanda ukauza. Kadhalika unaweza kutumia kiwanja ulichonunua kama dhamana pale unapotaka kuchukua mkopo.
Hivyo pia ndivyo ulivyo uwekezaji kwenye hisa, tofauti ni kwamba hisa unaweza kupata kwa bei ya chini kuliko kiwanja, na pia unaweza kununua na kuuza haraka kuliko kiwanja.

Zifuatazo ni faida tano nilizokuchagulia za kuwekeza kwenye ununuzi wa hisa. Nasema nilizokuchagulia kwa sababu faida zipo nyingi mno, huwezi kumaliza zote. Ila kwa hizi tano, utapata mwanga mkubwa sana.
- Njia ya uwekezaji.
Kununua hisa ni moja ya njia za uwekezaji, ambapo unaweka fedha yako mahali, inaendelea kukua kadiri muda unavyokwenda. Hapa unaweza kununua hisa zako na kuacha uwekezaji wako huo ukue kadiri muda unavyokwenda. Huhitaji kuwa na elimu kubwa hapa, wala mtaji mkubwa sana. unaweza kuchagua baadhi ya kampuni ambazo unaona zina uwezo wa kudumu, kisha kununua hisa zake na kutulia nazo.
- Njia ya kupata dhamana.
Unaponunua hisa, unaweza kutumia hisa zako kama dhamana ya kupata mikopo kwenye taasisi mbalimbali za kifedha. Hivyo kwa njia hii unaweza kupata fedha za kufanya uzalishaji mwingine, kwa kutumia dhamana ya uwekezaji wako.
- Kuuza na kununua kwa faida.
Ununuaji wa hisa unaweza kuufanya kama biashara, ambapo unanunua zikiwa bei chini na kuuza zikiwa bei juu. Hili litahitaji elimu na uzoefu mkubwa kidogo. Na mara nyingi linapelekea mtu kupata hasara. Lakini ni moja ya njia ya kufanya biashara kama mtu unavyonunua na kuuza vitu vingine.
- Njia ya kuweka akiba kama huna nidhamu.
Kuweka akiba nyumbani au benki kama huna nidhamu kuna changamoto moja, unaweza kuzitumia bila ya mpangilio. Unaweza kusema utatumia wakati wa dharura, halafu ukatengeneza dharura yako mwenyewe na kujikuta umetumia. Kwa sababu fedha ikiwa rahisi kuifikia, huwa haikosi matumizi. Lakini ukiweka fedha zako kwenye ununuzi wa hisa, siyo rahisi kuzitoa mara moja unapozitaka kama unavyoenda na kadi yako kwenye mashine ya ATM. Utahitaji kwenda kujaza fomu ya kuuza hisa, hisa ziwekwe sokoni, mauzo yafanyike ndiyo upewe fedha. Kama huna dharura kweli, hutafanya mchakato huo wote. Japo unahitaji kuwa na fedha kiasi kwa ajili ya dharura, lakini akiba ambayo hutaki kuitumia haraka, unaweza kuiweka kwenye hisa.
- Urahisi wa kuuza na kununua ukilinganisha na uwekezaji mwingine.
Zipo aina mbalimbali za uwekezaji, ukichukua mfano wa kiwanja tulioanza nao, ukitaka kununua kwanza lazima utafute kiwanja, pili uhakikishe ni halali kweli, bado uangalie kama bei unayoambiwa ni halali au la. Kwenye kuuza pia unaweza kusubiri sana mpaka upate mteja aliye tayari kununua. Lakini uwekezaji wa hisa upo tofauti kidogo, unapotaka kununua au kuuza ni rahisi, kulingana na upatikanaji na uhitaji wa watu. Pia huwezi kulanguliwa bei au kutapeliwa kwenye ununuzi wa hisa.
Faida hizi tano zinakupa sababu ya kwa nini uwekeze kwenye hisa. Zipo nyingine kama kuweza kuanza na kiasi kidogo cha mtaji na kuendelea kukua kadiri muda unavyokwenda. Ni muhimu kufanya uwekezaji kwenye hisa, ili kuweza kunufaika na ukuaji wa mtaji wako, hasa kwa siku za mbeleni.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
Ahsante sana Kocha,
Vip kuhusu utendaji wa kazi kwa upande wa madalali wa soko la hisa DSE,
Je ni vigezo vipi mtu unatakiwa kuzingatia pindi unapo chagua madalali wa kuwa tumia kwenye soko la hisa?
LikeLike
Nimejibu swali hili kwenye makala hii; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2017/09/28/uwekezaji-leo-dalali-wa-soko-la-hisa-ni-mtu-wa-aina-gani-na-jinsi-ya-kuchagua-dalali-mzuri/
LikeLike