Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?

Hongera sana kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo, ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu ANKDIKA AU UTASAHAU…

Akili zetu huwa zinakuwa na mawazo mengi sana kwa siku. Katika mawazo hayo yapo mengi ambayo siyo bora na machache sana ambayo ni bora kweli.

Changamoto kubwa ni kwamba, yale mawazo ambayo ni bora, usipokuwa na njia ya kuyavuna, yanapotezwa na yale mawazo ambayo siyo bora.

Hapa ndipo unapohitaji kuwa na mfumo ambao ni mzuri wa kuyavuna yale mawazo bora, kuyahifadhi na kuweza kuyatumia pale yanapofaa.

Njia bora ya kufanya hivyo ni kuandika yale mawazo bora. Na kwa kuwa mawazo bora yanaweza kukujia popote unapokuwa, unahitaji kuwa na kijitabu cha kuvuna mawazo yako hayo bora popote ulipo.

Unapopata wazo lolote ambalo ni bora au linaweza kuwa bora, unaliandika kwenye kijitabu chako hapo hapo. Usijiambie kwamba utakuja kuandika baadaye, mara nyingi unasahau na kupoteza mawazo hayo mazuri.

Faida nyingine ya kuandika ni kuelewa zaidi. Mara nyingi unapopata wazo huwa linakuwa halijakaa vizuri, unapoliandika, akili yako inapangilia vizuri na kuweza kulielewa vizuri sana.

Usikubali kupoteza mawazo yako mazuri kwa kukosa kijitabu cha kuyaandika. Popote ulipo, kuwa na kijitabu ambacho utakitumia kuandika mawazo yako bora, la sivyo utakuwa unayapoteza mara zote.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz