Hizi Ndiyo Sababu Kuu Tano Za Wewe Kuwa Na Bima Kwenye Uwekezaji Wako Wa Majengo.

Majanga mbalimbali yanayowakumba baadhi ya watu kwenye jamii zetu huacha alama na makovu makubwa kwenye maisha yao. Ukweli ni kwamba huwezi kufahamu uzito na maumivu ya matatizo ya mwingine hadi pale tatizo litakapokufika na namna utakavyolipokea. Uwekezaji wa majengo unakabiliwa na hatari nyingi zinazoweza kuangamiza uwekezaji wako kwa haraka na pasipo kutarajia. Hatari hizo zinaweza kusababishwa na chanzo cha asili au kutokana na matumizi ya kibinadamu ya majengo hayo. Imekuwa kawaida kusikia na kuona wamiliki wengi wakilia na kuteseka na familia zao, baadhi ya wawekezaji wakipata maradhi yanayotokana na mvurugano wa akili, mbaya zaidi ni kwamba baadhi hupoteza maisha wakati au muda mfupi baada ya kukumbwa na majanga. Hii inatokana na ukweli kuwa uwekezaji wa majengo hutumia muda na fedha nyingi katika kufikia malengo yake, hivyo kutokuwa tayari au kufanya maandalizi dhidi ya majanga ni tatizo letu la kifikra na kukosa maarifa dhidi ya kukabiliana na majanga. Majanga ya moto, mafuriko, kimbunga na wizi huweza kumkuta yeyote na pasipo kutarajia au kujipanga kwa namna yoyote, njia pekee ni kuwekea kinga uwekezaji wako kupitia kampuni mbalimbali za bima zinazojihusisha na kinga za mali na majengo dhidi ya majanga mbalimbali.

majengo30

KINGA DHIDI YA MAJANGA ASILIA

Ukweli ni kwamba hakuna aliye na uhakika na utayari wa kupambana na majanga ya asili pale yanapotokea. Majanga ya asili hutokea pasipo na taarifa, moto, mafuriko na vimbunga huwa na madhara makubwa sana kwenye majengo na mali zilizomo. Majengo ya kisasa yana mifumo ya kisasa inayotoa huduma kwenye majengo kwa ajili ya matumizi ya biashara na wakazi wake. Mifumo hii pia inaweza kuwa chanzo cha majanga kwenye majengo. Mifumo ya umeme, gesi, mawasiliano, muziki, usalama na maji inapaswa kukaguliwa mara kwa mara ili isiwe chanzo cha majanga yatakayo kunyima utulivu wa akili. Taasisi na kampuni za bima zipo kukufanya wewe uwe na amani dhidi ya msongo wa mawazo pale majanga ya asili yanapokutokea. Ni muhimu sana ukafanya tathmini na kufahamu hatari ambazo zina uwezekano mkubwa kutokea kwenye uwekezaji wako wa majengo na ukafanya maamuzi ya kuwatembelea wakala wa bima kwa ushauri na huduma zaidi. Kupitia bima utahakikishiwa makazi salama baada ya ajali na kufidiwa uharibifu wa mali yote uliyoiwekea bima kabla ya majanga kutokea.

SOMA; Usiruhusu Makosa Haya Yawe Sababu Ya Kuuza Kiwanja Au Nyumba Yako

KINGA DHIDI YA WIZI

Wakati tulionao sasa ni wakati muhimu sana wa kufanya mambo yetu kwa ufanisi na uhakika zaidi. Katika kufikia malengo yetu tunajikuta tunanunua vifaa na mashine mbalimbali za gharama ambazo zinatusaidia katika kurahisisha maisha yetu na kuyafanya yawe ya furaha na amani. Fikiria umerudi na unapata taarifa kuwa mali zote za uzalishaji mali zimeibwa, hakika utapokea taarifa hii kwa namna ambayo hukutarajia, kwa ufupi utapatwa na mshituko utakaokuletea mfadhaiko wa akili na mwili. Ili kukabiliana na hatari za namna hii ni vizuri ukaweka bima ya majengo na mali zake ili iwe kinga yako pale majanga yatakapo kukuta. Endapo mali hiyo itaibwa au kuharibiwa ni wajibu wa taasisi au kampuni ya bima kukuhakikishia fidia na uwezekano wa kupata mbadala ndani ya muda wa makubaliano. Kupitia bima daima akili yako itakuwa adui namba moja wa msongo wa mawazo na mfadhaiko wa akili pale mambo yatakavyoenda tofauti na matarajio kwenye uwekezaji wako.

UHAKIKA WA DHAMANA YA MKOPO

Kwa hapa Tanzania karibu watu wote niliopata kuwauliza sababu kuu ya wao kuwa na bima ya majengo na mali zilizomo ilikuwa ni msukumo kutoka taasisi ya fedha ili waweze kufanikiwa kupata mkopo utakao wasaidia kukidhi shughuli zao za kimaendeleo. Ni wachache sana walio na bima kwa hiyari yao wenyewe, na hata hawa wachache walijifunza kutokana na majanga yaliyowakuta watu wao wa karibu. Karibu taasisi zote za fedha hupokea majengo yote kama dhamana ya mkopaji endapo itakuwa na bima itakayo hakikisha usalama na uwepo wa dhamana hiyo. Wawekezaji wengi kukopa fedha ni sehemu ya maisha yao ya ukuaji kibiashara na uwekezaji wanaoufanya, hivyo bima ni msaada na njia ya uhakika itakayokuhakikishia usalama wa majengo yako na kwa taasisi ya fedha kujiridhisha usalama wa dhamana yako pasipo na shaka ya aina yoyote. Bima itakuwa pamoja na wewe kuhakikisha unapata utulivu wa akili endapo utapatwa na majanga wakati ambao bado upo kwenye kipindi cha mkopo. Jifunze kuwa na bima kwa hiyari yako, nyumba ni mali na thamani yake hukua siku hadi siku.

NGAO BORA KWENYE MAJANGA YA KISHERIA

Kwenye uwekezaji wako wa majengo ni muhimu kuwa na bima yenye kinga dhidi ya majanga ambayo utahitaji msaada wa kisheria pale ambapo utapatwa na majanga yanayohitaji msaada wa kisheria ili kunusuru uwekezaji wako wa majengo. Ni muhimu sana ukajihakikishia usalama wa nyumba yako na mali zilizomo kwa kuwa na bima nzuri yenye kukujali na kukuhudumia vizuri pale utakapo hitaji msaada ili kuzuia uwezekano wowote wa kupoteza nyumba yako endapo hiyo ni mali yako pasipo na shaka ya aina yoyote. Ni muhimu sana tukaanza kuweka utamaduni wa kufahamu umuhimu wa bima kwenye uwekezaji wetu wa majengo tofauti na tulivyo sasa. Hali hii itasaidia watu wengi kuwa na uhakika wa usalama kwa kile walichowekeza kwa muda mrefu katika kufikia ndoto zao. Watembelee wataalamu wa bima, wapo kwa ajili yako kukuhudumia na kukupa ushauri wa usalama wa mali zako.  Ongeza thamani ya uwekezaji wako kwa kuwa na bima itakayokuwa pamoja na wewe wakati wote wa maisha yako ya ukuaji kwenye biashara na uwekezaji.

SOMA; Mambo Matatu Ya Kuzingatia Kabla Ya Kufanya Uwekezaji Wa Majengo Ili Uepuke “Bomoabomoa”

KINGA DHIDI YA MFADHAIKO WA AKILI

Lengo kuu la bima duniani kote ni kushughulika na dharura zinazojitokeza ndani ya jamii, mara nyingi imejikita kwenye mambo yaliyo kwenye mahitaji muhimu kwa matumizi na maisha ya mwanadamu lakini yapo kwenye hatari kubwa inayoweza kutokea wakati usiofahamika au pasipo kujiandaa. Ni ukweli kuwa wakati mwingine majanga hujitokeza na usijue nini cha kufanya, hali hii itakufanya ukose amani na matumaini ya kuendelea kuishi kutokana na namna utakavyolipokea tatizo dhidi ya uwezo wako hafifu wa kupambana na tatizo hilo. Mara nyingi tumejikuta katika hali ya msongo wa mawazo na mfadhaiko wa akili pale majanga yanapotukuta na hatuna mbadala wa nini cha kufanya ili maisha yaendelee kama ilivyokuwa mwanzo. Njia pekee ni kuwa na bima yenye uhakika wa kukuhudumia wakati wote wa dharura ili maisha yako yawe na thamani. Mfadhaiko wa akili huondoa thamani halisi ya wewe kuishi hapa duniani. Mafanikio ya kweli kwenye uwekezaji wa majengo ni wewe kuwa na amani na furaha wakati wote wa maisha yako.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

 

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com

One thought on “Hizi Ndiyo Sababu Kuu Tano Za Wewe Kuwa Na Bima Kwenye Uwekezaji Wako Wa Majengo.

Add yours

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: