Tupo kwenye wakati usiotabirika katika hali zote za kimaisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya kiuchumi. Mabadiliko ya hali ya uchumi ni jambo mtambuka ambalo hugusa maisha halisi ya watu kuanzia kwenye tabaka binafsi, familia, taifa na dunia kwa ujumla wake. Hali ya uchumi inapo badilika husababisha ukuaji au kudorora kwa maendeleo ya jamii husika. Kukua au kudorora kwa uchumi wa taifa kunapimwa kwa kuangalia viashiria mbalimbali vikiwemo ukuaji wa pato la taifa, mfumuko wa bei, thamani ya fedha za ndani, mwenendo wa sekta za kibenki na akiba ya fedha za kigeni na huwa na athari za moja kwa moja kwenye maisha halisi ya watu. Katika hali yoyote ya kiuchumi tuliyonayo maisha bado yataendelea na tunapaswa kuishi maisha yanayoendana na hali ya uchumi wa wakati huu.

Hali ngumu ya kiuchumi ni jambo ambalo husababisha hofu na wasiwasi kwenye jamii inayohitaji kupata unafuu wa maisha ili kuboresha maisha yao, hivyo ni muhimu sana kujipanga ili uweze kukabiliana na hali yoyote ya kiuchumi katika kutimiza malengo yako. Changamoto nyingi za kibiashara, kielimu, kiafya na uwekezaji wowote huongezeka wakati wa hali ngumu ya kiuchumi.

majengo 38

Haijalishi unataka kuwekeza kwenye kilimo, ufugaji, majengo, huduma za jamii, misitu, viwanda au usafirishaji bado hautapuuza kuhusu hali halisi ya uchumi kwenye jamii yako. Leo nitakupa baadhi ya mbinu ambazo ukizizingatia utakuwa mmoja kati ya wachache ambao wanachukua hatua mbalimbali kuelekea kwenye uwekezaji wa ardhi na majengo pamoja na kupitia hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili.

Itambue Hali Yako Ya Kipato.

Pale unapogundua kuwa hali yako ya kiuchumi inabadilika na inazidi kuwa ngumu zaidi hupaswi kuishi kwa wasiwasi au woga, bali unapaswa kutenga muda wa kujitathimini upya hali yako ya kifedha. Ni muhimu sana ukaifahamu vizuri hali yako na mwenendo wa mapato na matumizi ya kifedha na kuamua  kubadili mbinu mpya ya kuzalisha fedha ili kuendana na mabadiliko ya hali ya uchumi kwa wakati huu. Ukishaitambua hali yako ya kipato itakuwezesha kufanya maamuzi ya hekima na busara yatakayokusaidia kutimiza malengo yako kwa ufanisi mkubwa hata kama upo kwenye hali ngumu ya kiuchumi, wakati mwingine inakulazimu utumie muda mwingi tofauti na ulivyozoea ili kukabiliana na changamoto za wakati huu. Wakati huu ndio wakati bora zaidi wa kuanza kufanya uwekezaji kwa kuwa ni watu wachache sana wenye uwezo wa kupambana na hali ya soko kwenye hali ngumu ya kiuchumi. Kwa kila kidogo unachokipata na kukifanyia kazi ndicho kitakacho kusaidia kukupeleka kwenye mafanikio makubwa ambayo hautayafikia endapo utaweka visingizio mbalimbali vya kushindwa. Ungana na wachache ambao wameamua kwa dhati kutimiza malengo yao katika hali yoyote ile watakayokutana nayo kwa kuwa wana tabia ya kubadilika kutokana na mwenendo wa hali zote za kiuchumi. Wekeza kulingana na kipato chako.

SOMA; Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kuepuka Hatari Na Hasara Kwenye Uwekezaji Wa Ardhi Na Majengo.

Badili Mfumo Wako Wa Maisha.

Ni muhimu sana kujitathimini mwenendo wa maisha yako ya kila siku ili uweze kumudu hali ngumu ya kiuchumi na wakati huohuo kutimiza malengo yako ya kuwa huru kifedha. Ni jambo jema sana endapo utapunguza gharama za kimaisha kwa kuepuka kushughulika na mahitaji yasiyo na ulazima au umuhimu kwa wakati huu. Hapa unahitaji kuwa na ujasiri wa hali ya juu sana kwa kuwa wengi wetu hujitengenezea hofu isiyojulikana mbele ya jamii. Kwa kufanya hivyo utakuwa umejipunguzia mzigo mkubwa wa msongo wa mawazo ambao kwa kiasi kikubwa ulitokana na matumizi mengi ya mambo yasiyo na ulazima. Ongeza bidii ya kazi unayoifanya, boresha huduma zako kwa jamii na mwisho weka juhudi kwenye kuweka akiba ambayo itakuwezesha kufanya uwekezaji ambao utakufanya kuwa huru kifedha kwa siku chache zijazo. Epuka kuwa na fedha nyingi ambazo hazizalishi fedha za ziada, hicho kidogo unachopata kitumie sasa kuanza uwekezaji wa ardhi na majengo ambao thamani ya uwekezaji hukua kadri muda unavyosonga mbele tofauti na uwekezaji mwingine.

Weka Bidii Kuboresha Mtandao Wako.

Pale unapokabiliana na hali ngumu ya kiuchumi unahitaji kuzitambua fursa nyingi kwa kadri inavyowezekana kupitia watu mbalimbali, unahitaji sana kujenga mtandao mkubwa wa watu wenye manufaa ili kuweza kutambua fursa mbalimbali kupitia mtandao huo, Jambo kubwa hapa ni kufanya juhudi ya kuwa na wateja wengi zaidi ambao utawashawishi uweze kuwahudumia na kutatua matatizo yao kwa ufanisi mkubwa na kwa upande mwingine kwako inakuwa ni fursa ya kuongeza kipato ambacho kitakusaidia kuboresha maisha yako. Tumia mbinu za kisasa zaidi ambazo zitakuwezesha kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi na zinazoendana na wakati. Kwa kufanya hivyo itakuwezesha kuwa na maisha bora hata kama utakuwa unapitia kwenye hali ngumu ya kiuchumi. Kufanikiwa kwa maisha yako kutakufanya uwe mtulivu wa mwili na akili hali itakayokufanya uanze hatua mbalimbali za uwekezaji wa ardhi na majengo kutegemea na malengo ambayo umeshajiwekea. Pia kupitia mtandao wako ni rahisi kupata taarifa na maarifa sahihi yatakayo kusaidia kutimiza ndoto yako na kuanza uwekezaji ukiwa na uhakika wa kile unachokwenda kufanya.

Epuka Madeni Mapya.

Ni muhimu sana ukawa makini kwenye mapato dhidi ya matumizi yako ya kila siku, mwezi na hata mwaka mzima. Unapokabiliana na hali ngumu ya kiuchumi ni rahisi sana kujitokeza kwa changamoto za dharura ambazo zinaweza kuathiri hali yako ya kifedha, hali hii inapokutokea usikate tamaa bali unapaswa kuendelea kwa kuanza na pale ulipoishia jana. Wakati huu ni muda muafaka wa kupunguza madeni mbalimbali na kwa upande mwingine unajitahidi kuepuka madeni mapya kutokana na kutotabirika kwa hali ya kipato, pia si vema ukawa mwepesi wa kukimbilia mkopo kwenye taasisi za fedha kwa kuwa huweka riba kubwa hali ambayo itakufanya kuwa mtumwa endapo mambo yataenda tofauti na matarajio yako. Kuepuka madeni mapya kutakuweka kwenye hali nzuri ya wewe kuanza kujiwekea akiba na hata kuanza uwekezaji mpya. Kwenye hali ngumu ya kiuchumi kuna wengine wanafanikiwa zaidi na wengine wanaangamia kwa haraka sana, tofauti kubwa inatokana na mtazamo wa kila mmoja na hatua atakazochukua katika kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi.

SOMA; Hizi Ndiyo Sababu Kuu Tano Za Wewe Kuwa Na Bima Kwenye Uwekezaji Wako Wa Majengo.

Badili Mbinu Za Mpango Kazi.

Wakati tulionao mambo mengi yanabadilika kwa haraka sana tofauti na matarajio yetu, mabadiliko haya yanatulazimisha kuanza kufikiri tofauti kwenye kila jambo katika kukabiliana na mfumo mpya wa maisha.  Fikra na mbinu nyingi zilizotumika siku za nyuma hazina nguvu tena kwa sasa, mabadiliko haya ndiyo yatakayoamua kukuangusha na kushindwa kuendelea na safari ya mafanikio au kuendelea na safari yako ya mafanikio endapo utakuwa na dhamira ya dhati ya kubadilika ili kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi. Ifikirie upya kazi yako, biashara yako na huduma mbalimbali unazotoa kama zitakusaidia kuboresha maisha yako na kukupa fursa ya kuanza uwekezaji wa ardhi na majengo ambao kwa kiasi kikubwa upo imara kwenye hali zote za kiuchumi tofauti na uwekezaji mwingine. Nguvu ya kuanza uwekezaji unakuja pale unapoweza kuwa mwepesi wa kubadilika, kwa kubuni njia mpya na bora za kukabiliana na hali ya ushindani wa masoko kwenye kila unachokifanya bila hofu na wasiwasi wa kushindwa.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com