Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu SAHIHI NA KWELI…
Kama kitu siyo sahihi, usifanye, hata kama kila mtu anafanya, hata kama wanaofanya wananufaika. SIYO SAHIHI, USIFANYE.
Kufanywa na wengi na hata wanaofanya kunufaika haibadilishi kitu ambacho siyo sahihi kuwa sahihi. Kitabaki kutokuwa sahihi na siku moja mambo yote yatakuwa wazi.
Kama kitu siyo kweli, usiseme, hata kama kila mtu anasema, hata kama ni siri unamwambia mtu. SIYO KWELI, USISEME.
Usiseme kabisa kile ambacho siyo kweli, usiseme ambacho umesikia na hujadhibitisha. Usiseme habari za mtu kwa mwingine, ambapo yeye mwenyewe hatofurahia.
Hata kama unasema kwa siri kiasi gani, kama siyo ukweli unaosema na kama haikuhusu, ipo siku ulichosema kitakuwa na madhara kwako.
Tukizingatia mambo hayo mawili, SAHIHI na UKWELI, tutapunguza nusu ya matatizo na changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha yetu ya kila siku.
Mara zote fanya kile ambacho ni sahihi, hata kama uko peke yako na hakuna anayekuona.
Mara zote sema ukweli, hata kama kusema hivyo unapoteza fursa.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.