KITABU; Philosophy for life and other dangerous situations : ancient philosophy for modern problems / Jules Evans
UKurasa 153 – 166

Wanafalsafa ambao wanapingana na mifumo ya kijamii iliyopo, CYNICS wanatuonesha ni kwa namna gani ustaarabu na kutaka kuonekana vizuri kwa wengine kulivyo mateso kwetu.
Kupenda kwetu kufanya kile ambacho wengine wanafanya, na kuonekana tupo vizuri kwa wengine, kumetengeneza watu wenye maisha yanayoonekana vizuri nje lakini ndani ni mateso matupu.

Cynics wanasema kwamba ukiangalia mfumo kama wa ubepari, unastawi kupitia mateso ya watu. Tamaa za watu kutaka vitu vizuri ambavyo hawana uwezo navyo, wanaenda kukopa ili wavipate, mkopo huo wanaulipa kwa riba, hivyo inawabidi kufanya kazi zaidi kulipa mkopo na kuendesha maisha pia.
Na hata baada ya mtu kupata kile ambacho alikuwa anakitaka sana, anagundua kuna kizuri zaidi ya kile, ambacho ni bei ghali kuliko hicho. Hapo anakazana tena kufanya kazi akipate, na hata kuingia kwenye madeni.
Ni tamaa hizi za watu ndiyo zinafanya mfumo wa ubepari kufanya kazi.

Kuna usemi kwamba watu wanatumia fedha ambazo hawana (MIKOPO) kununua vitu ambavyo hawavihitaji ili kuwaonesha watu ambao hawajali.

Mmoja wa mwanafalsafa aliyekuwa Cynic, Diogenes alikuwa mpingaji mkubwa wa mifumo hii. Aliainisha kwamba maisha mazuri hayahitaji vitu vingi ambavyo watu wanapigania kupata.
Hakuwa na nyumba, mali yoyote, wala mke au watoto.
Alikuwa na gunia la kulalia, alilala mitaani na kula mabaki ya chakula na kusema ana furaha kuliko wanaoteseka kupata mambo makubwa ambayo hawana muda wa kuyafurahia.

Japokuwa hii ni falsafa ngumu kuiishi kwenye maisha, kipo cha kujifunza, kwamba chochote tunachopigania kwenye maisha yetu, je kina maana kwetu au tunataka tu kuonekana na wengine?
Ni kweli upo ulazima wa wewe kukopa nguo mpya ilihali unazo nguo nyingine unaweza kuvaa mpaka pale utakapopata fedha ya kununua?
Ni kweli kwamba unahitaji kukopa fedha ufanye sherehe kubwa?
Ni kweli unahitaji kuchukua mkopo mkubwa ujenge nyumba kubwa na ulipe mkopo huo maisha yako yote?
Tukijiuliza maswali ya aina hii, tutaweza kufanya maamuzi sahihi na kufanya kile ambacho kina maana kwenye maisha yetu na siyo tu kufanya ili kuonekana na wengine.