Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?

Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo mazuri sana.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Leo tutafakari kuhusu MBIO ZA PANYA…

Kwenye maisha yetu, vipo vitu ambavyo tunafanya, zipo juhudi ambazo tunaweka, lakini mwisho wake tunabaki pale pale tulipo.

Yaani licha ya kuweka juhudi fulani, matokeo yake hayabadilishi chochote kwenye maisha yetu.

Hizi ndiyo mbio za panya, kwa sababu hata unaposhinda mbio hizo, unabaki kuwa panya. Hakuna mabadiliko yoyote.

Kwa mfano pale mtu unapokuwa na changamoto za kifedha, halafu ukaamua kuchukua hatua kama ya kwenda kukopa, unaweza kupata fedha kwa mkopo, lakini changamoto yako ya fedha ipo pale pale, na huenda ikawa mbaya zaidi.

Au mtu una changamoto ya kimaisha, na kuamua kwenda kutumia kilevi ili uisahau, changamoto inabaki pale pale.

Unafanya kazi au biashara yako kwa njia zile zile, hakuna ubunifu unaoweka, hakuna la ziada unalofanya, halafu unategemea uongeze kipato chako, hizo ni mbio za panya.

Kwenye mbio za panya, hatua unazokazana kuchukua ni bure kwa sababu hazikutoi pale ulipo na kukupeleka mbele zaidi.

Tafakari maisha yako kwa kina, tafakari kila unalofanya na jiulize je upo kwenye mbio za panya?

Ukishagundua upo kwenye mbio za panya, basi hatua ni kuondoka haraka, kwa sababu hakuna muujiza unaoweza kukutokea ukiwa kwenye mbio za panya.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz