Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari na kutahajudi KISICHOWEZA KUSUBIRI NUSU SAA…

Kwa maisha bora ya kiroho kwako, unahitaji muda wa kuwa na wewe mwenyewe kila siku.

Huu ni muda ambao wewe mwenyewe unakaa na wewe mwenyewe, ukisali, kutahajudi, kutafakari na hata kupitia ndoto zako kubwa za maisha.

Ni muda ambao unapaswa kuwa tulivu sana kwako, usio na usumbufu wa aina yoyote, na inapaswa kuwa kila siku.

Lakini cha kushangaza, wengi wetu tumekuwa hatupati muda wa aina hii kwenye siku zetu.

Siku zetu zimejaa na kubanana kiasi kwamba tunaona kutenga nusu saa kwa ajili ya hilo ni kupoteza muda.

Na hapa ndipo ninapotaka tujiulize, je ni kitu gani hicho tunafanya na maisha yetu ambacho hakiwezi kusubiri nusu saa?

Je tunafanya kazi ya kuzima moto na muda wote kuna moto wa kuzima?

Au sisi ni askrari wa dunia, ambao kila dakika lazima tuwe pembeni ya simu zetu, la sivyo, dunia itaanguka?

Au ukitenga nusu saa isiyokuwa na usumbufu kwako, ya kukaa na wewe mwenyewe, kuna watu wengi watakufa kwa kukosekana kwako kwa muda huo?

Ni kipi hicho kwenye maisha yetu ambacho hakiwezi kabisa kusubiri kwa nusu saa?

Tutafakari na kujiuliza swali hili leo na kila siku, na tuone kama yafaa kutenga nusu saa kwenye siku yetu kwa zoezi hili muhimu kiroho na kimafanikio pia.

Lakini kama tutaona maisha yetu hayawezi kumudu kupata nusu saa hiyo muhimu, kwamba tuna mengi ya kufanya na tusipoyafanya basi dunia itasimama kabisa, litakuwa ndiyo chaguo letu.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz