Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu DAKIKA TANO…
Tutafakari dakika tano za maisha, dakika tano za utulivu na dakika tano za udhibiti wa maisha yetu.
Kwa sehemu kubwa tumekuwa tunaishi maisha kwa kujibu kile kinachotutokea. Labda ni mtu amesema na kuuliza kitu na hapo mawazo yetu yanakuwa kwenye mfumo wa kujibu kitu hicho. Au ni habari tulizopokea na zinatawala mawazo yetu.
Kinachotokea ni kwamba kwa siku nzima, akili yako inakuwa imetawaliwa na mawazo mbalimbali, ambayo huna udhibiti nayo.
Sasa ili kuweza kurejesha udhibiti huu, unahitaji dakika tano tu…
Katika dakika hizi tano, fanya yafuatayo;
Nenda sehemu ambayo imetulia, sehemu ambayo haina kelele, hakuna atakayekuja hapo na usiwe na simu.
Kaa vizuri na funga macho yako,
Anza kupumua ukihesabu pumzi zako. Ukivuta pumzi ndani hesabu moja, ukitoa nje hesabu mbili, endelea hivyo mpaka ufike kumi.
Kisha anza tena kuhesabu moja mpaka kumi.
Fanya zoezi hili kwa dakika tano tu, kisha ondoka na endelea na shughuli zako.
Zoezi hili litakusaidia sana kutawala akili zako, kushinda wasiwasi na hofu na kuweza kutuliza mawazo na kufikiri kwa kina.
Na hili ni zoezi la kawaida kabisa, halitegemei dini au imani yako, wala halihitaji useme sala ya aina yoyote. Unachofanya ni kupumua kwa kina, kitu ambacho ni muhimu sana kwenye maisha yetu.
Tumia dakika tano leo kufanya hilo zoezi, fanya tena kesho na kila siku. Ukiweza dakika tano ongeza muda zaidi, kama dakika tano ni nyingi anza hata na dakika tatu.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.