Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa sana.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu UNACHOPATA..

Watu wengi huwa wanastuka na kuchukua hatua kutokana na kile wanachopata.

Lakini hatua wanazochukua huwa hazileti mabadiliko yoyote kwenye kile wanachopata.

Na hii ni kwa sababu wanakuwa hawajui misingi muhimu ya kile mtu anachopata.

Kile unachopata ni matokeo ya fikra ambazo zimetawala akili yako.

Na kile unachopata ndiyo ulichoridhika kupata, umekubaliana nacho na ni matokeo ya juhudi ulizoweka.

Hivyo basi, kama unachopata hakikuridhishi, kabla hujachukua hatua angalia kwanza ni fikra zipi ulizonazo juu ya matokeo unayopata?

Kama kipato ulichonacho ni kidogo, tafakari kwenye fikra zako umejiwekea wewe thamani kubwa kiasi gani kifedha? Kwa sababu watu watakulipa kile unachokubali ni thamani yako.

Pia angalia juhudi unazoweka, kama hazijachangia kile ulichopata.

Kutaka kubadili matokeo bila ya kubadili misingi mikuu ya fikra na kuridhika kwako, ni sawa na kukata matunda yanayojitokeza kwenye mti wa maembe ili yatoke machungwa. Haifanyi kazi.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz