Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUZALISHA…
Katika hii dunia, unaweza kuwa MZALISHAJI au ukawa MLAJI…
Lakini watu wengi wamechagua kuwa walaji, na siyo wazalishaji.
Watu wengi wanapenda kufanya kile ambacho tayari kimeshafanywa, na siyo wao kukaa chini na kufanya.
Hali hii inazalisha watu wengi ambao ni tegemezi kwa watu wachache.
Hii ni kuanzia kwenye kazi, biashara, maisha, mahusiano, burudani na kadhalika.
Watu wengi wanapenda kutumia muda wao kufuatilia vile vya wengine, kuliko kutumia muda huo kufanya vya kwao.
Watu wengi wanapenda wengine wawape furaha, badala ya wao wenyewe kujitengenezea furaha.
Maisha yetu yanakuwa na maana pale tunapozalisha, pale tunapofanya kitu kwa manufaa ya wengine.
Je ni vitu gani unazalisha kwenye kila eneo la maisha yako?
Acha kuwa mlaji pekee, na anza kuwa mzalishaji, kwenye kila eneo la maisha yako. Hakikisha watu wananufaika na uwepo wako, na siyo kuona uwepo wako kama mzigo au mteja pekee.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.