Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?

Ni siku nyingine nzuri sana hii, ambapo tumepata nafasi nzuri na ya kipekee ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu SIKU YOYOTE NI SIKU YA KUANZA…

Watu wengi wamekuwa wanapanga mambo mazuri ya kufanya kwenye maisha yao, ila huona mipango hiyo inafaa kuanzwa kwa siku ya kipekee.

Labda mtu anapanga na kusema nitaanza mwaka mpya,

Au anapanga na kusema nitaanza mwanzo wa mwezi ujao,

Mwingine atapata wazo zuri la kufanya siku ya jumamosi na kusema nitaanza siku ya jumatatu.

Ninachotaka kukuambia rafiki yangu ni hichi, kama kuna kitu unataka kufanya, kama kuna wazo bora umepata, basi siku nzuri ya kuanza ni siku hiyo hiyo.

Usiache wazo lako lipoe, usiache ile hamasa ya mwanzo ipungue.

Anza kufanya hata kama ni kwa hatua ndogo, halafu andaa mazingira ya kuendelea kufanya.

Hakuna tofauti kwenye siku bali fikra unazokuwa umeweka.

Hivyo inapokuja swala la kuchukua hatua ya kuboresha maisha yako, wakati wowote ni wakati mzuri kwako kuanza.

Anza sasa, anza leo na yafanye maisha yako kuwa bora zaidi kila siku.

Hatua ndogo ndogo unazochukua kila siku zina mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yako.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz