Rafiki,

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya USHAURI WA CHANGAMOTO mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Unapokutana na changamoto siyo mwisho wa safari, bali ni hatua ya kukua zaidi. Hivyo wajibu ni kutatua changamoto ili kuweza kusonga mbele zaidi.

Tunaishi kwenye zama ambazo kila kitu kinabadilika na mabadiliko haya yanatokea kwa kasi sana. Miaka kumi iliyopita kila mtu alikuwa anafikiria kuwa kwenye ajira ya kudumu, lakini sasa ajira za kudumu ni kama ndoto.

Na hili limepelekea watu wengi zaidi kujitegemea kwenye kipato, hivyo kuingia kwenye biashara siyo tena kitu cha kujiuliza uingie au la. Bali kila mtu anapaswa kuwa na biashara, iwe umeajiriwa au la, biashara ni muhimu.

Lakini biashara zina changamoto zake, wengi wanaingia kwenye biashara na kuishia kupata hasara na kushindwa. Leo kwenye makala hii ya ushauri nakwenda kukushirikisha mbinu za kuweza kuendesha biashara yenye mafanikio na kuepusha biashara kufa.

Kabla hatujaingia kwenye mbinu zenyewe, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili;

Sijui jinsi ya kuendesha biashara, naanza vizuri lakini najikuta mtaji umeshuka kila ninapojitahidi nashindwa hata kutunza akiba. – Flora K. N

Kama alivyotuandikia msomaji mwenzetu Flora hapo, wapo watu wengi ambao wanaingia kwenye biashara, mambo yanakuwa mazuri mwanzoni lakini baadaye mambo yanaanza kwenda vibaya.

kuzabiashara

Haya hapa ni mambo matano muhimu ya kuzingatia ili kuweza kuendesha biashara yenye mafanikio makubwa na kuepusha biashara kushindwa.

Moja; itenganishe biashara yako na wewe mwenyewe.

Kosa kubwa ambalo watu wengi wanafanya ni kufikiri kwa sababu wameanzisha biashara, basi wao ni biashara zao na biashara zao ni wao. Ukienda hivi lazima utashindwa kwenye biashara.

Biashara yako ni mtu tofauti na wewe ni mtu tofauti. Kila mmoja ana maisha yake ila tu mna uhusiano wa karibu.

Hivyo usitumie fedha za biashara kama vile ni fedha zako binafsi, na wala usichukue vitu kwenye biashara kama vile ni vitu vyako binafsi.

Kama unaitegemea biashara yako kwa kipato, basi jilipe kwa mahesabu, labda kiasi fulani kwa siku, wiki au mwezi, au kujilipa sehemu ya faida. Usitoe fedha yoyote kwenye biashara kwa matumizi binafsi, hata kama una dharura. Unapaswa kuwa na fungu la dharura.

Kama unafanya biashara ambayo vitu vyake unaweza kuvitumia mwenyewe, usijichukulie tu kama unavyotaka, bali chukua kwa kununua, ujikate kwenye malipo yako unayotengeneza kwenye biashara yako.

Ukiweza kupiga hatua hii ya kwanza, utakuwa umetatua tatizo kubwa linaloua biashara nyingi.

Mbili; dhibiti mzunguko wa fedha kwenye biashara yako.

Fedha ndiyo damu ya biashara, kama itapotea, biashara lazima ife. Biashara yoyote inayopoteza fedha, haiwezi kujiendesha kwa muda mrefu. Hivyo hili ni eneo muhimu na unalopaswa kuwa makini nalo.

Kwanza kabisa jua matumizi muhimu kwenye biashara yako, na epuka kabisa matumizi ambayo siyo muhimu. Usitumie tu fedha za biashara hovyo, utaiua.

Pili ongeza mapato kwenye biashara yako kwa kuongeza mauzo, labda kwa kuongeza wateja wapya au kuongeza bidhaa na huduma zaidi.

Tatu, epuka kukopesha, tengeneza wateja ambao wanalipia fedha taslimu. Kukopesha ni moja ya sababu za biashara nyingi kupunguza mtaji na kufa. Ni bora ubaki na bidhaa kwenye biashara ambayo hujaiuza, kuliko kukopesha halafu usilipwe, maana hapo unakuwa umepoteza mtaji.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE SMALL BUSINESS BIBLE (Kila Kitu Unachopaswa Kujua Ili Kufanikiwa Kwenye Biashara Ndogo).

Tatu; tengeneza wateja waaminifu kwenye biashara yako.

Biashara za sasa ni mahusiano, hasa katika zama hizi ambapo mteja anafuatwa kule alipo. Hivyo unahitaji kutengeneza mahusiano mazuri na wateja wako, kutengeneza wateja ambao ni waaminifu kwa biashara yako.

Chagua tatizo au hitaji unalowatimizia wateja wako, kisha weka juhudi kuhakikisha wateja wanapata kilicho bora kabisa. Hakuna mteja ambaye hapendi ubora, ukiwapa ubora, watakuja zaidi na zaidi.

Toa huduma nzuri sana kwa wateja wako, wajali, wasaidie kutatua changamoto zao na pia washauri vizuri sana. Yote haya yanawafanya wateja kukuona upo kwa ajili yao na wanapokuwa na uhitaji wa kile unachouza, watakufikiria wewe tu.

Kamwe usiendeshe biashara yako kwa mazoea, usifanye kwa sababu umezoea kufanya, fanya kwa sababu kuna mchango mkubwa unaotoa.

Nne; usikimbilie mikopo kwa sababu umeambiwa unakopesheka.

Tumekutana na wafanyabiashara wengi wanaosema biashara zao zilikuwa zinaenda vizuri kabla hawajachukua mkopo, lakini baada ya mkopo, mambo yamekuwa magumu.

Kwanza kabisa usichukue mkopo kuanza biashara mpya, kwa sababu utaanza kulipa marejesho kabla biashara haijaanza kutengeneza faida, hivyo utakuwa unapunguza mtaji.

Pili, hata kama biashara tayari inajiendesha vizuri, usichukue mkopo kwa sababu tu umeambiwa unakopesheka. Bali chukua mkopo pale ambapo una mahali pa uhakika pa kuuweka kwenye biashara yako na ukazalisha faida ndani ya muda mfupi ili uweze kulipa vizuri.

Tatu, kama utachukua mkopo, basi utumie kwa lile kusudi ulilochukulia pekee. Usiutumie kwa mambo mengine, hata kama ni muhimu kiasi gani. Kuwa na nidhamu.

SOMA; Namna Unavyoweza Kukuza Biashara Yako Hadi Kufikia Utajiri.

Tano; kuwa na mpango wa ukuaji wa biashara.

Kitu cha mwisho ninachokwenda kukushirikisha hapa ambacho kinawazuia wengi kufanikiwa kwenye biashara, ni kukosa mpango wa ukuaji. Watu wengi wanakuwa kwenye biashara kwa mazoea, wanafanya kwa sababu jana walifanya na kesho wanaendelea kufanya tena.

Hawana picha yoyote kibiashara miaka 10, 20 mpaka hata 50 ijayo.

Biashara yoyote unayofanya sasa, au uliyopo, jua ni hatua unapita. Unahitaji kwenda ngazi za juu zaidi kwenye biashara hiyo, au kwenda biashara nyingine ya ndoto zako.

Kwa vyovyote vile, usiridhike na kuona kama umeshafika, biashara zinabadilika na changamoto ni nyingi. Kuwa na mpango wa ukuaji wa biashara unaoufanyia kazi kila siku.

Fanyia kazi mambo hayo matano kwenye biashara yako, na baada ya muda utaanza kuona mabadiliko makubwa kwenye biashara yako na maisha yako pia. Endesha biashara yako kibiashara, na siyo kimazoea, na kadiri biashara inavyokua, utahitajika kukua zaidi kifikra.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog