Moja ya uwekezaji kwenye masoko ya mitaji ni kununua hatifungani, ambapo unaikopesha fedha kampuni au taasisi kwa makubaliano ya kulipwa kwa riba.
Watu wengi wamekuwa hawaelewi vizuri uwekezaji huu wa hatifungani, kwa sababu hauongelewi sana na kwa hapa Tanzania, hatifungani zinazopatikana sokoni siyo nyingi kama hisa.

Leo nakwenda kukushirikisha faida tano za kuwekeza kwenye hatifungani, ili uweze kufikiria hili katika mipango yako ya uwekezaji.
- Uwekezaji salama.
Hatifungani ni moja ya uwekezaji salama unaoweza kufanya. Hii ni kwa sababu wewe unakuwa umeikopesha kampuni au taasisi, hivyo hata kama itapata hasara au kufa, wewe utapaswa kulipwa deni lako na riba ambayo mlikubaliana.
Tofauti na hisa ambapo mtu anakuwa kwenye hatari ya kupoteza uwekezaji wake pale lolote linapotokea.
- Riba kubwa ukilinganisha na benki.
Unaweza kuweka fedha benki, hasa kwenye akaunti za muda maalumu, lakini riba zake huwa ni ndogo. Ukiwekeza kwenye hatifungani, unapata riba kubwa ukilinganisha na benki.
Kwa mfano kwa benki, riba kwa wasatani inaweza kuwa asilimia 3 mpaka asilimia 5. Wakati hatifungani zinakuwa na wastani wa riba ya asilimia 7 mpaka asilimia 10.
- Uhakika wa riba.
Uwekezaji kwenye hatifungani unaleta uhakika wa riba ambayo mtu unapata ukilinganisha na uwekezaji kwenye hisa ambapo huwezi kujua kwa uhakika ni kiasi gani unapata.
Unaponunua hatifungani, unajua kabisa ni kiasi gani cha riba utapata kila mwaka.
SOMA; UWEKEZAJI LEO; Tofauti Ya Uwekezaji Kwenye Hisa Na Hatifungani.
- Uwekezaji wa muda mrefu.
Hatifungani nyingi ni za muda mrefu, kuanzia miaka mitano na kuendelea. Zipo mpaka za miaka 15 na nchi nyingine miaka zaidi ya 30. Hii inafanya hatifungani kuwa uwekezaji wa muda mrefu, kwa wale ambao wanapenda fedha zao zikae na kuzalisha kwa muda mrefu.
- Dhamana ya mkopo.
Unaweza kutumia uwekezaji wako kwenye hatifungani kama dhamana ya kupata mkopo kwenye taasisi mbalimbali za kifedha. Kwa njia hii unapata fedha ya kuzalisha, kupitia fedha zako ulizowekeza. Unaona hili lilivyo na faida, unanufaika mara mbili.
Hizi ndizo faida za kuwekeza kwenye hatifungani, ambapo kubwa ni usalama wa uwekezaji na uhakika wa kipato. Lakini ukilinganisha na uwekezaji kwenye hisa, anayepata faida kwenye hisa inakuwa kubwa kuliko hatifungani, lakini hasara kwenye hisa inakuwa kubwa pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog