Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?

Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo.

Ni fursa nzuri na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo mazuri sana.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu MISINGI YAKO ITAJARIBIWA..

Utakapochagua kuishi maisha yanayoendeshwa na misingi ya maisha ya mafanikio, jambo moja unalopaswa kufahamu ni kwamba, misingi yako itajaribiwa.

Utapata tamaa ya kwenda kinyume na misingi hiyo, japo kwa muda mfupi.

Tamaa hii inaweza kuanzia ndani yako, kwa kuona unajitesa sana na misingi hiyo, na kuona labda ukikwepa msingi mmoja utapata unachohitaji haraka.

Tamaa hii pia inaweza kutoka nje, kutokana na mazingira na wale wanaokuzunguka, ukashawishika kwamba ukienda kinyume na misingi yako, kuna kitu kizuri utakipata, au utawahi kupata unachotaka.

Kabla hujakubaliana na ushawishi huo wa kwenda kinyume na misingi yako, kumbuka kwamba misingi haina huruma. Misingi inafanya kazi, ukiifuata unapata matunda mazuri, ukiivunja unapata matunda mabaya, hata kama utapata mazuri ndani ya muda mfupi.

Usikubali kabisa ushawishi wa kuvunja misingi yako, endelea kuiishi, endelea kuisimamia kama sehemu ya maisha yako. Unapokutana na majaribu, usikubali yakuingie na kukupotezea muda wako.

Mara zote fanya kile ambacho ni sahihi, mara zote ishi kulingana na misingi ya asili ya maisha na misingi uliyojiwekea. Tofauti na hapo ni kupoteza muda.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz