Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kutegemea kupata makubwa.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu PUMUA KWANZA…
Kwenye maisha yetu huwa tunakutana na hali ambazo hatukuzitegemea,
Inawezekana ni mtu kukuudhi, au mipango yako kwenda tofauti na ulivyotaka au pia inaweza kuwa ajali fulani.
Hali zote hizi hufanya miili yetu kuingia kwenye hali ya KUJIKINGA NA KUPAMBANA. Ambapo mwili mzima unabadilika, unajijengea tahadhari kubwa na kuwa tayari kupambana na lolote.
Tahadhari hii ya mwili huwa ni kubwa kuliko kile tulichokutana nacho, na huwa inatuzuia kufikiri kwa makini.
Kwa kifupi mwili wako unapoingia kwenye hiyo hali yatahadhari, huwezi kufikiri kwa makini. Ndiyo maana unaweza kufanya jambo halafu baadaye ukaja kujutia kwa nini ulifanya vile.
Sasa ili kuepuka kufanya mambo yasiyo sahihi, unahitaji kudhibiti mwili wako pale unapoingia kwenye hali ya tahadhari.
Na njia bora ya kufanya hivi ni kupumua kwanza….
Unapokuwa kwenye hali yoyote ya taharuki, changamoto au hasira, usikimbilie kuchukua hatua yoyote ya haraka, badala yake pumua kwanza.
Achana na chochote unachofikiria au kutaka kufanya na PUMUA.
Vuta pumzi ndani na toa pumzi nje, ukihesabu pumzi zako na kusikiliza jinsi hewa inavyopita kwenye pua zako mpaka kwenye mapafu yako.
Iweke akili yako kwenye pumzi yako, pumua kwa kina, pumua kwa undani.
Fanya hivyo kwa angalau dakika tano,
Matokeo yake yatakuwa bora sana.
Akili itatulia,
Hasira zitashuka,
Mwili utarudi sawa,
Na utakuwa umeepuka kufanya maamuzi ya hovyo.
Unapokuwa kwenye hali yoyote ambayo hukuitegemea au ya kukukasirisha, PUMUA KWANZA, zoezi hilo litakuwezesha kufanya maamuzi bora.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.