Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu DUNIA HAIENDI HIVYO…
Mara nyingi watu wanavurugwa na kukasirishwa na vitu ambavyo vipo kabisa nje ya uwezo wao.
Unakuta mtu anataka kila kitu kiende kama anavyotaka yeye,
Apate kila kitu kwa wakati anaotaka yeye, na kwa namna anayotaka yeye.
Kila mtu awe kama anavyofikiria yeye, afanye kile ambacho yeye anataka.
Watu wanapenda kudhibiti kila kitu kinachotuzunguka.
Lakini hilo linashindikana, na mtu anakosa furaha, anajisikia vibaya pale kila kitu kinapokuwa hakiendi kama anavyotaka yeye.
Ninachotaka kukukumbusha asubuhi hii rafiki yangu ni kwamba DUNIA HAIENDI HIVYO…
Dunia haiendi kama wewe unavyotaka, bali inaenda kama inavyotaka yenyewe.
Vitu vingi unavyotaka, vipo nje ya uwezo wako, na hata vile unavyofikiri vipo ndani ya uwezo wako, ni kwa kiasi pekee.
Hivyo kuwa tayari kukosa kile unachotaka,
Kuwa tayari kuwaruhusu watu kuwa vile wanavyotaka kuwa,
Na kubali kwamba huwezi kudhibiti kila kitu.
Fanya kwa nafasi yako, kisha ipe dunia nafasi ya kufanya kwa nafasi yake.
Wakati mwingine utakosa, wakati mwingine utachelewa na wakati mwingine utapata.
Hivyo ndivyo dunia inavyokwenda, siyo kwa vile unavyofikiri na kutaka wewe, bali kwa namna inavyoenda yenyewe.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.