Habari za leo rafiki yangu?

Kuiona siku nzuri kama hii ya leo ni jambo la kushukuru sana, kwa sababu siyo kila mtu amepata nafasi kama hii ambayo tumeipata mimi na wewe. hivyo tunapaswa kuheshimu sana muda huu wa kipekee, tuutumie vyema kwa mafanikio yetu na ya wale wanaotuzunguka.

Leo katika kipengele hichi cha nyeusi na nyeupe ambapo nimekuwa nakupa ukweli kama ulivyo, hata kama utakuumiza, nakwenda kugusia mfano wa michango ya harusi na jinsi tunaweza kutumia mfano huo kufanikiwa zaidi.

Nilipata nafasi ya kufikiri hili kwa kina  baada ya ujumbe niliotoa wiki hii, katika jumbe fupi fupi ninazotoa kwa njia ya picha kupata maoni ya msomaji. Ujumbe huo ni huo nimeweka kapo chini. Ambapo niliandika; Watu wangekuwa wanakusanya michango ya biashara kwa nguvu kama wanavyokusanya michango ya harusi, tusingesikia tatizo la ukosefu wa mtaji kwenye biashara.

Michango

Mmoja wa wasomaji aliniandikia maoni yake na kusema; tatizo la jamii yetu ni kwamba watu wanapenda na wapo tayari kuchangia harusi lakini siyo kuchangia biashara.

Kwa haraka nilikubaliana naye, kwa kukumbuka kuwa jamii yetu watu wanapenda sana kufanya vitu vyenye matokeo ya haraka kuliko vinavyohitaji  muda kuleta matokeo. Lakini baadaye nikasema hivi ni kweli?

Ni kweli kwamba watu wanachangia harusi kwa sababu wanapenda? Na hawachangii watu kuanza biashara kwa sababu hawapendi?

Ni katika kujihoji huku ndipo nilipofanya utafiti mdogo sana kuanzia na mimi mwenyewe na watu ninaowafahamu. Na katika utafiti huu nimegundua kitu kimoja kikubwa sana, ambacho kila mtu akiweza kukitumia, ataweza kupiga hatua kubwa sana na hakuna atakayemrudisha nyuma.

Nilichogundua ni kwamba, hakuna mtu yeyote anayependa kuchangia harusi, hakuna kabisa. Sijawahi kukutana na mtu anasema nina hizi kadi tano za harusi hapa, ni raha iliyoje kuwachangia watu wote hawa watano, nafanya hivyo mara moja.

Kila mtu analalamika wingi wa michango ya harusi, watu wana kadi nyingi za kuchangia harusi kuliko hata uwezo wa kipato chao. Lakini pamoja na kutokupenda na malalamiko hayo ya watu, harusi zinachangiwa kila siku. Hata yule ambaye hapendi kuchangia, mwisho wa siku anachangia.

SOMA; Licha Ya Vikwazo Unavyokutana Navyo Kung’ang’ana Kwako Kunamfundisha Mwingine, Usichoke.

Je nini kinasababisha hili kutokea? Nini kinawasukuma watu kuchangia harusi licha ya kutokupenda kuchangia?

Na jibu lipo wazi kabisa, usumbufu, ung’ang’anizi na kutokukata tamaa kwa wale wanaokusanya michango ya harusi. Hakuna watu waliojitoa na wasioogopa chochote kama watu ambao wanakusanya michango ya harusi zao, au za watu wa karibu kwao.

Ni watu ambao wanakuwa ving’ang’anizi kweli, kwanza watawasiliana na kila mtu ambaye wanamfahamu, hata kama walimjua kupitia rafiki. Halafu watatuma ujumbe mara kwa mara mpaka mtu utachoka kupokea ujumbe huo na kuamua ulipie tu mchango ili mtu asijisikie vibaya.

Wakati mwingine unaona jinsi mtu anavyojitoa kukutafuta, kuwasiliana na wewe na kukukumbusha mpaka unaona umchangie tu ili aweze kukamilisha shughuli yake.

Wakati mwingine mtu anakuwa anakufanya uone huruma kabisa, hasa changamoto na msongo wanaopitia katika ukusanyaji wa michango hiyo. Na hata kama hukuwa na mpango wa kuchangia, unaona utoe tu kama kumuunga mkono, hasa kama ni mtu wa karibu na ambaye mna mahusiano ya karibu.

Sasa hayo niliyoeleza hapo juu, ndiyo yanayokosekana kwenye aina nyingine za michango.

Tuangalie machango wa kuanzisha biashara kwa mfano. Watu wengi huwa na uhitaji wa mitaji ya kuanza au kukuza biashara zao. Hupata wazo la kuongea na ndugu, jamaa na marafiki ili wawachangie mtaji huo. Lakini wanapowaambia, watu hao huwa na sababu, labda hawapo vizuri, au mambo yao yamebana na majibu mengine yanayofanana na hayo.

Kinachotokea ni mtu anakubaliana na sababu hizo, na kutulia, akikubali kwamba watu hawana fedha za kumchangia mtaji wa biashara.

Sasa kabla hujakubaliana na majibu hayo, muulize mtu yeyote ambaye amewahi kuchangisha mchango wa harusi. Kuna kikao cha ahadi, ambapo watu wanaahidi, lakini hawatoi hapo hapo. Ni mpaka wafuatiliwe sana, wakumbushwe kukamilisha ahadi zao, wasumbuliwe mpaka wao wenyewe wajisikie vibaya ndiyo waweze kutoa michango hiyo.

Hivyo ninachotaka kukuambia hapa rafiki yangu ni kwamba, watu wengi huwa wanakosa kile wanachotaka kwa sababu hawang’ang’ani vya kutosha. Wanakubali haraka pale wanapoambia haiwezekani au hawawezi kupata walichoomba. Hawawi wasumbufu vya kutosha, hawawafanyi watu wawe na msukumo wa kuwachangia kutoka ndani yao.

Kwa kifupi watu wanakuwa waoga na wenye aibu sana wanapoomba kitu kutoka kwa wengine. Wanakuwa hawapo tayari kuvumilia kusubiri na kuendelea kuwakumbusha watu mpaka wapate kile wanachotaka.

SIRI KUBWA YA MAFANIKIO YA KUJIFUNZA HAPA.

Ipo siri kubwa sana ya mafanikio tunayoweza kujifunza kupitia mfano huu wa michango ya harusi. Na siri hiyo ni ung’ang’anizi, uvumilivu na kutokukata tamaa.

Chochote unachotaka kwenye hii dunia, jua kwamba hutakipata kirahisi, naweza kukuhakikishia hilo. Utakutana na vikwazo vya kila aina, utakutana na kuchelewa kwa mambo uliyofikiri utayapata haraka.

SOMA; Jinsi Ya Kutokukata Tamaa Katika Nyakati Ngumu Za Maisha.

Kama hujajitoa kung’ang’ana na kuvumilia bila ya kukata tamaa, utaishia njiani. Utaona mambo hayawezekani, utaona wale waliofanikiwa labda wana kitu cha ziada ambacho wewe huna. Lakini ukweli ni kwamba, wamepitia kila unachopitia wewe, lakini hawakukubali kukata tamaa.

Popote ulipo sasa, hata kama ni pagumu kiasi gani, hata kama huoni mbele, hata kama mambo yanaonekana hayawezekani tena, napenda nikupe moyo kwamba huo siyo mwisho. Ni njia ya dunia kukujaribu, kuona umejitoa kiasi gani kupata hicho unachofikiri unakitaka.

Tumia mfano huu wa wanaokusanya michango ya harusi kupata chochote unachotaka, ondoa aibu, acha kufikiria watu watakuchukuliaje, fanya lililo sahihi, wafuatilie watu kwa karibu ili kupata chochote unachohitaji.

Muhimu kabisa, tengeneza mahusiano yako na wengine vizuri, usiwe mtu wa kutaka kupata tu kutoka kwa wengine, bali kazana kutoa zaidi kwa wengine. Wape wengine thamani kubwa, jitoe kwa ajili ya wengine, na wao watakuwa na kila sababu ya kukupa kile unachotaka.

Ng’ang’ana, kuwa mvumilivu, kuwa na subira na usikate tamaa. Hakuna njia ya mkato kwenye hili, utakutana na mengi ya kukuzuia, lakini wewe pekee ndiye unayeweza kuyashinda na kupata kile unachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

MIMI NI MSHINDI

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog