Huwa nasema mtu wa kwanza kuchukua ushauri wake kuhusu wateja wa biashara yako ni wewe mwenyewe.
Na unafanya hivyo kwa kuangalia huduma unazopata kutoka kwa wafanyabiashara wengine pale unapokwenda kupata huduma mbalimbali, hata kama haziendani na biashara yako.
Kila mmoja wetu, huwa anapata hisia fulani anapokwenda kwenye biashara nyingine. Huenda ni kufurahishwa na kuridhishwa sana na huduma zinazotolewa. Au kuchukizwa na kutoridhishwa na huduma ambazo unakuwa umepata.

Kwa hisia zozote ambazo unapata unapokuwa unapata huduma kwenye biashara mbalimbali, ondoka na somo ambalo unakwenda kutumia kwenye biashara yako. Kama umefurahishwa, jifunze kipi kimekufurahisha na kakitumie kwenye biashara yako. Kama hukufurahishwa jifunze kipi ambacho hakikuenda vizuri na usikitumie kwenye biashara yako.
SOMA; BIASHARA LEO; Maswali Matatu Muhimu Kujiuliza Kuhusu Wateja Wa Biashara Yako.
Na siyo lazima huduma uwe umeipata wewe ndiyo ujifunze, unaweza kuangalia wateja wengine pia namna wanavyopata huduma na namna wanavyozichukulia kisha ukajifunza kitu cha kwenda kufanyia kazi kwenye biashara yako.
Aliyekuwa mfanyabiashara na bilionea wa Marekani, Sam Walton, mwanzilishi wa maduka ya Wal-Mart, alisifika kwa kwenda kwenye maduka mengine na kuangalia namna watu wanavyonunua. Inasemekana hata akiwa mzee aliwahi kukamatwa kwenye duka akifikiriwa ni mwizi, kutokana na kukutwa akipima urefu wa shelfu la kuweka bidhaa. Alijifunza kwenye kila aina ya biashara na kuondoka na kitu cha kufanyia kazi kwenye biashara zake.
Hii ni fursa nzuri kwa kila mmoja wetu kujifunza na kuboresha biashara zetu. Kwa kuangalia namna tunavyopokea huduma kwa wengine na namna watu wengine wanavyohudumiwa kwenye biashara nyingine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog