Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nzuri na ya kipekee sana kwetu, siku ambayo tumepata nafasi ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JE UNAWEZA KUDHIBITI?
Yapo mambo mengi ambayo yanatokea kwenye maisha yetu.
Na mambo haya tunaweza kuyagawa katika makundi mawili;
Kundi la kwanza ni mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu, mambo tunayoweza kuyadhibiti, mambo ambayo tunaweza kuchukua hatua na tukaleta mabadiliko fulani.
Kundi la pili ni mambo ambayo yapo nje ya uwezo wetu, mambo tusiyoweza kuyadhibiti, mambo ambayo hakuna hatua tunayoweza kuchukua ikaleta mabadiliko yoyote.
Watu wengi wamekuwa wakisumbuka na kushindwa kuchukua hatua kwa sababu hawachukui hatua ya kugawa mambo wanayopitia.
Wanalalamikia mambo wasiyoweza kudhibiti, huku wakilaumu wengine kwa mambo wanayoweza kuyadhibiti.
Sasa suluhisho la uhakika ni hili;
Unapokutana na jambo lolote kwenye maisha yako, jiulize swali moja; je naweza kudhibiti jambo hili? Je lipo ndani ya uwezo wangu?
Kama jibu ni ndiyo, chukua hatua mara moja kuweza kubadili jambo hilo.
Kama jibu ni hapana, basi achana nalo na songa mbele kwa kufanya yale yaliyopo ndani ya uwezo wako.
Kamwe usipoteze muda kwa kulalamikia jambo lolote, au kumlaumu yeyote au kusubiri labda mambo yatakuwa mazuri.
Chukua hatua kwa yaliyopo ndani ya uwezo wako na achana na yaliyopo nje ya uwezo wako.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.