Karibu kila mtu ana mpango fulani ambao anataka kuufanyia kazi kwenye maisha yake.
Watu wengi wanajua nini wanapaswa kufanya kwenye maisha yao, kazi yao, biashara yao na maeneo mengine.
Na hata wasiojua, wana wazo kwamba pale walipo sasa bado hapawatoshi na kuna mambo yanayofanywa na wengine ambayo wanatamani na wao wangefanya.
Lakini inapofika wakati wa kufanya, wengi husita kuanza kufanya. Wengi huona bado hawajakamilika na kuwa tayari, huona watakosea na hivyo kuharibu.
Hivyo huchagua kusubiri mpaka pale watakapokuwa tayari ili wakianza, waanze kwa uhakika na kupata kile wanachotaka.
Wote tunajua mawazo ya aina hii huwa yanaishia wapi, mtu hachukui hatua kabisa. Kwa sababu ni vigumu sana mtu kuwa tayari na kukamilika kwenye kila eneo la maisha yake.

Tunaishi kwenye jamii ambayo inatukuza mafanikio yanayoonekana kwa nje na kupuuza kushindwa ambako kunatengeneza mafanikio hayo. Hivyo kila mtu anaogopa kukosea na kushindwa, kwa kuona ni aibu, ni dhambi kubwa.
Ninachotaka kukukumbusha leo ni kwamba, dhambi kubwa kabisa kwenye maisha yako siyo kukosea au kushindwa. Kwa sababu kwa jambo lolote utakalochagua kufanya kwenye maisha yako, kuna mahali utakosea, kuna mahali utashindwa.
SOMA; UKURASA WA 456; Umekosea…
Lakini kukosea au kushindwa siyo mwisho, badala yake ni njia ya kujifunza. Ni kiashiria kwamba kuna vitu vya kuboresha zaidi ili kuweza kupata kile unachotaka.
Dhambi kubwa kabisa kwenye maisha yako ya mafanikio ni kutokuchukua hatua yoyote, kukaa na kusubiri mpaka mambo yawe mazuri au mpaka uwe umekamilika.
Hii ni dhambi kubwa kwa sababu hakuna chochote unachojifunza kama huchukui hatua. Hata kama unasoma na kuwaangalia wengine, hiyo ni sehemu ndogo sana na haidumu. Unachohitaji ni kuchukua hatua, kufanya na kujifunza kwa vitendo, kupitia kukosea na kushindwa.
Kama kwa kuchukua kwako hatua utakosea au kushindwa, unaweza kubadili na kuboresha zaidi, lakini kama utakaa na kusubiri mpaka uwe tayari ndiyo uchukue hatua, hakuna hatua yoyote utakayopiga.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog