Bilionea Bill Gates amewahi kuandika kwenye moja ya vitabu vyake kwamba mteja ambaye hajaridhishwa ni sehemu kubwa sana ya kujifunza kwenye biashara. Akiwa na maana kwamba, kama kuna mteja ambaye hajaridhishwa na huduma au bidhaa uliyomuuzia, ni mteja ambaye atakufundisha mengi sana.
Ni jambo lisilo na shaka kwamba katika kuwahudumia kwetu wateja, baadhi ya wateja hawataridhishwa na huduma walizopata. Wakati mwingine ni kwa sababu zao binafsi, labda kuwa na matarajio makubwa kuliko uhalisia. Lakini wakati mwingine ni kwa sababu zetu sisi wafanyabiashara.

Kuna makosa ambayo unaweza kuyafanya, yakapelekea mteja kukosa huduma au bidhaa aliyokuwa anataka. Au akaipata lakini isimsaidie kama alivyotegemea.
Huu ni wakati mzuri kwako kujifunza na hata kurudisha imani ya wateja wako.
Unachoweza kujifunza hapo ni jinsi ya kutatua changamoto hizo za wateja na kujua kipi kimepelekea changamoto ya aina hiyo kutokea na kuweza kuhakikisha haitokei tena wakati mwingine.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kujenga Biashara Kubwa Ya Wateja Wanaolipa Fedha Taslimu Na Siyo Mikopo.
Unachoweza kufanya kujenga zaidi imani ya mteja wako ni kutatua changamoto hiyo kwa manufaa ya mteja, hata kama wewe unapata hasara. Hapa unaweka maslahi ya mteja mbele, hivyo kumsaidia mpaka apate kile anataka, hata kama inakugharimu wewe.
Kwa kuchukua hatua ya aina hii, mteja ataridhishwa sana na kuona ana deni kubwa kwako, hata kama wewe ndiye uliyekosea.
Hii ni kwa sababu wateja huwa wanakosa imani ya kusaidiwa pale wanapopata changamoto. Wafanyabiashara wengi wana mtazamo wa kwamba nikishakuuzia basi kinachotokea ni juu yako, hainihusu. Lakini wewe unapochukua hilo na kuwa juu yako, mteja anajenga imani kubwa kwako na ataendelea kuwa mteja wako kwa muda mrefu.
Kama lengo lako ni kuwa kwenye biashara kwa muda mrefu, kama unafikiria miaka 100 ijayo ya biashara yako, basi weka maslahi ya wateja wako mbele. Wakati mwingine kuwa tayari kuingia hasara kuhakikisha mteja anapata alichotaka au ulichomwahidi atapata.
Mteja aliyeangushwa au ukatishwa tamaa na huduma au bidhaa aliyopata kutoka kwenye biashara yako, ni mteja mzuri kujifunza na pia kujenga uaminifu wake kwako pale unapotatua changamoto yake hiyo.
Kumbuka wapo wateja wasumbufu, na wengine wanatengeneza matatizo ili wanufaike, hivyo busara yako inahitajika katika kufanya maamuzi yoyote ya biashara yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog