Watu wengi wamekuwa wakipata hasara kwenye uwekezaji kwa sababu hawatumii akili zao kutafuta maarifa sahihi na kufanya maamuzi sahihi. Badala yake wamekuwa wakitegemea wengine wawafanyie hivyo. Wamekuwa wakisubiri wengine wawaambie nunua hisa hizi, utapata faida kubwa na kadhalika.
Wengi wanabeba ushauri huo kama ulivyo, wananunua hisa fulani, au kuwekeza eneo fulani lakini hawapati ile faida waliyotegemea kufanya. Hapa ndipo hulaumu uwekezaji au wale ambao waliwashauri kuwekeza.

Kama unataka kuwa mwekezaji bora, ambaye unanufaika na uwekezaji, basi kuna aina ya watu unapaswa kuwaepuka sana katika uwekezaji.
Watu hao ni wale wanaokuhakikishia kwamba uwekezaji fulani utakupa faida baadaye. Mtu yeyote anayetabiri chochote kwenye uwekezaji, unapaswa kumwepuka. Kwa sababu katika historia ya uwekezaji, hakuna yeyote ambaye amewahi kutabiri kwa asilimia 100 ya usahihi mara zote.
SOMA; Sheria Tano Muhimu Za Kufuata Wakati Wa Kuchagua Hisa Za Kununua.
Uwekezaji wa aina yoyote ile una hatari zake, hatari hizi zinatofautiana kulingana na aina ya uwekezaji. Lakini hatari haiwezi kuwa haipo kabisa.
Hivyo unapochukua hatua ya kuwekeza, jua kabisa kwamba lolote linaweza kutokea, unaweza kupata faida na unaweza kupata hasara. Hivyo ni wajibu wako kujifunza njia za wewe kupunguza nafasi ya kupata hasara, ikiwepo kuwekeza maeneo mbalimbali na tofauti.
Mtu yeyote anayekuhakikishia ukiwekeza eneo fulani kuna uhakika wa kupata faida, basi anakudanganya. Huenda kuna namna ananufaika kwa wewe kuchukua hatua, au hajui tu, huenda na yeye ameambiwa hivyo anavyokuambia wewe.
Ni vizuri kupata ushauri kuhusu uwekezaji, lakini pia unapaswa kuchukua muda wa kujifunza, kutafiti na kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji.
Usipende ushauri rahisi na unaoweza kutolewa na kila mtu kuhusu uwekezaji. Hoji na nenda ndani zaidi ili uweze kufanya maamuzi sahihi kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog