Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza mtandao unaoongoza kueneza habari hasi kwa kasi zaidi kuliko yote duniani je unaujua ni mtandao gani? hivyo basi,  karibu tujifunze.

Habari za hofu zimekuwa nyingi kuliko habari nyingine, kiufupi habari hasi zimeshika chati kila kona ya jamii yetu. kama ni kwenye mitandao ya kijamii basi hizi habari hasi ndiyo zimekuwa zikipewa kipaumbele kuliko zote. Watu wanaweka juhudi na kutaka kuwa wakwanza kuonekana na yeye amepost juu ya tukio fulani bila kujali ni salama kwa watu au la.

Rafiki, ukitaka kukata tamaa haraka katika maisha yako na kuona maisha yako wewe hayana maana basi ni kwenye mitandao hii ya kijamii. Utajiona kabisa wewe hakuna unachofanya ila wengine ndiyo wanafanya sasa na wale ambao hawaujui ukweli ndiyo wanapata shida katika maisha yao, ile hali ya kwenye mitandao ya kijamii inakuwa inawatesa kiakili na hatimaye kuwa watumwa wakubwa. Hii mitandao ya kijamii ni biashara za watu na imebuniwa ili wewe uendelee kuitembelea zaidi ili kuwaingizia kipato.

habari hasi mtandaoni

Leo hii ikitokea habari ya ajali au ya mchawi katika jamii yako na nyingine kuhusiana na kitu chochote cha mafanikio yaani chanya basi ile ya ajali au ya mchawi ndiyo itavuma na kuenezwa kwa kasi zaidi kupita maelezo. Watu wanakua vinara wa kusambaza zile habari  hasi kwa watu wengi zaidi bila kujali hiyo habari italeta matokeo gani katika maisha ya mtu. Unaweza kukuta mtu anaanza siku yake kwa kuanza kusikiliza habari  na anakutana na habari hasi ambayo inamvunja nguvu na hamasa ya kwenda kufanya makubwa ndani ya siku husika.

Unakuta mtu ameanza siku kwa unyonge baada ya kupokea habari hasi zilizoua hamasa yake na kuona kabisa hii dunia si sehemu salama kwani habari hasi zimemjaza hofu ya kutokuona umuhimu wa kuendelea kuishi katika hii dunia. Sasa swali letu la kujiuliza na ndiyo shabaha yetu leo ni mtandao gani huo unaoeneza  habari kwa kasi zaidi kuliko yote duniani? Jibu ni kwamba mtandao huo siyo mwingine bali ni wewe mwenyewe. Hakuna mtandao unaojiongoza na kusamabaza habari bila ya nguvu ya binadamu kufanya kazi.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Raising Positive Kids In A Negative World (Jinsi Ya Kulea Watoto Wenye Mtazamo Chanya Kwenye Dunia Hasi).

Ndugu msomaji, zile habari hasi tunazojiona zikisambaza kila siku katika mitandao ya kijamii hazijisambazi zenyewe ila sisi wenyewe ndiyo tunachangia kuzisambaza  habari hizo. Kama matukio hasi yakitokea na hakuna mtu anayechukua hatua za kusambaza matukio katika mitandao ya kijamii basi dunia itakuwa salama. Sisi wenyewe ndiyo mitandao inayoeneza habari hasi kwa kasi zaidi kwa sababu habari zenyewe haziwezi kujisambaza zenyewe kama upepo pasipo mtu kuchukua hatua ya kusambaza.

Hatua ya kuchukua leo, usiwe mtumwa wa kusambaza habari hasi ambazo hazimsaidii mtu na badala yake zinamuongezea matatizo tu. Kama hujaanza kusambaza habari kaa chini na jiulize habari hii ninayotaka kusambaza italeta matokeo gani chanya kwa watu? Ukiona haina matokeo chanya achana nayo na endelea na shughuli zako chanya. Usipoteze muda na nguvu kuharibu dunia bali tumia muda na nguvu kuifanya dunia yako kuwa sehemu bora ya kuishi.

Kwahiyo,tutaweza kupunguza matatizo mengi katika jamii yetu kama kila mmoja akiacha kwa makusudi kabisa kusambaza habari hasi katika mitandao ya kijamii. Kwani sisi wenyewe ndiyo mitandao mibaya ya kuharibu dunia, tunatumia nguvu na muda wetu vibaya kuhubiri na kusambaza habari hasi badala ya chanya. Hakuna mtandao unaoweza kutenda na kusambaza habari hasi bila ya wewe mwanamtandao wa kwanza kupeleka habari katika mitandao hiyo.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana.