Ukinunua kiwanja leo kwa shilingi milioni moja, halafu baada ya mwaka mmoja ukauza kiwanja hicho kwa shilingi milioni mbili, kuna ongezeko la thamani la mtaji ulioweka.
Wewe uliweka mtaji ambao ni shilingi milioni moja, lakini baada ya mwaka mtaji huo umekua na kufikia milioni mbili.
Ongezeko la thamani ya mtaji ni kitu muhimu sana kwenye uwekezaji kwa sababu ndiyo kinapima faida ya uwekezaji.
Kila aina ya uwekezaji una ongezeko lake la thamani ya mtaji.

Unaponunua hisa kwa bei ya chini, baada ya muda zikapanda bei, mtaji ulioweka unakuwa umekua zaidi. Hata unaponunua vipande au kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja kama UTT, vipande vinapopanda bei mtaji wako unakuwa umeongezeka thamani.
Jambo muhimu sana la kujua kwenye ongezeko la thamani ya mtaji, ni kwamba utahesabu pale unapouza. Hata kama bei imepanda, lakini hujauza na kupata fedha zako, huwezi kuhesabia kwa hakika kwamba mtaji wako umeongezeka.
Tukirudi kwenye mfano wa kiwanja, unaweza kununua kiwanja leo, kwa shilingi milioni moja, baada ya mwaka kiwanja kama chako kwa maeneo uliyopo kikawa kinauzwa milioni mbili. Au akaja mtu akakuambia niuzie kwa milioni mbili, na wewe ukakataa. Wengi huhesabu uwekezaji wao umekua thamani. Lakini linaweza kutokea jambo wakati huo huo na likafanya thamani hiyo ishuke kabisa. kwa mfano yakatokea mafuriko na eneo hilo likaharibiwa sana, ghafla bei inashuka na mtu hanunui hata kwa shilingi laki tano.
Hivyo pamoja na bei kuongezeka, unaweza kupima ongezeko la thamani ya mtaji wako baada ya kuwa umeuza uwekezaji wako.
Ongezeko la thamani ya mtaji linakatwa kodi.
Ongezeko la thamani ya mtaji katika uwekezaji huwa linakatwa kodi. Hivyo uwekezaji wowote unaofanya, unapaswa kujua kwamba ile thamani inayoongezeka kwenye mtaji ulioweka, inakatwa kodi.
Lakini kodi hii inakatwa pale unapouza uwekezaji huo. Hivyo thamani ikiongezeka lakini hujauza, hakuna kodi inayokatwa. Ila pale unapouza na kuona thamani halisi, hapo ndipo unapolipa kodi.
Hii ndiyo sababu ni muhimu kuwekeza maeneo ambayo yanakua vizuri na kwa muda mrefu, kuliko kununua na kuuza uwekezaji mara kwa mara kwa sababu kodi inaweza kuwa kubwa. Kodi zinatofautiana kwa aina ya uwekezaji. Lakini inaweza kufika mpaka asilimia 30 ya ongezeko la thamani hiyo ya mtaji wako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog