Nothing happens to any man that he is not formed by nature to bear. – Marcus Aurelius
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari; UMEANDALIWA KUKIKABILI…
Kila mtu anakutana na mambo makubwa sana kwenye maisha yake, ambayo hakutegemea kukutana nayo.
Inawezekana ni changamoto kubwa kabisa ambayo inakuja kwa wakati ambao mtu hukutegemea.
Mambo kama ugonjwa, hasara, kufukuzwa kazi na mengine makubwa, yanakatisha tamaa sana.
Watu wengi wanapojikuta kwenye changamoto hizi kubwa, hukata tamaa na kuona hawawezi tena. Huona huo ndiyo mwisho wao na wasijue nini wanaweza kufanya.
Ukweli ni kwamba, CHOCHOTE UNACHOKUTANA NACHO KWENYE MAISHA YAKO, UMEANDALIWA KUKIKABILI.
Hakuna kitu unachokutana nacho, ambacho huwezi kukikabili, ukikitana na kitu cha aina hiyo, ambacho huwezi kukikabili, wala hutajua ka,a umekutana nacho, kwa sababu hutapona.
Hii ina maana kwamba, hata kama unapitia changamoto kubwa kiasi gani, kama bado upo hai, basi huo siyo mwisho, bado ipo nafasi kwako kuchukua hatua tena.
Mazingira yamekuandaa uweze kutoka hapo, na ukiweza kuyatumia, basi utapiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.
Usiogope kupitia magumu, vikwazo au changamoto, vyote hivyo umeandaliwa kuvikabili, tumia kila kilichopo ndani yako kuhakikisha unavikabili na kuweza kupiga hatua.
Ukipata hasara haimaanishi elimu na uzoefu wako wote ulionao kwenye biashara umepotea, badala yake umeongeza uzoefu zaidi.
Ukifukuzwa kazi haimaanishi elimu yako, nguvu zako na uzoefu uliopata kwenye kazi hiyo vimechukuliwa. Bali ni uhuru wa kuwa bora zaidi.
Wakati wowote unapokuwa kwenye magumu na kuona unakaribia kukata tamaa, jikumbushe kauli hii; LOLOTE NINALOPITIA SASA, NIMEANDALIWA KULIKABILI, HIVYO NINALIKABILI NA NITAVUKA HAPA.
Nakutakis siku bora sana ya leo, nenda kayakabili yote unayokutana nayo leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa