Kaa Kwenye Kile Unachofanya Hata Kinapokuwa Kigumu…

Kila kitu unachopanga kufanya kwenye maisha yako, kuna wakati kinakuwa kigumu. Iwe ni kazi, biashara na hata maisha ya kawaida. Upo wakati utafikia ugumu na akili kuona haiwezi kwenda tena.

Huu ndiyo wakati ambapo wengi huwa wanatoroka, wanaacha kufanya kile walichokuwa wanafanya na kuingia kwenye usumbufu.

Tatizo kubwa zaidi ni kwamba, tunaishi kwenye dunia yenye kelele na usumbufu mwingi. Mitandao ya kijamii imekuwa sehemu ya wengi kukimbilia pale wanapokuwa wamekutana na ugumu au changamoto kwenye kazi wanazofanya.

mitandao

Kwa kuwa ni rahisi kuingia kwenye mitandao hii, wengi huigeuza kuwa kimbilio. Mtu anapanga kufanya kitu fulani, lakini katika kufanya anafika eneo ambalo ni gumu na linamtaka kufikiri kwa kina zaidi na kuweka juhudi zaidi. Hapo anatafuta kitu rahisi zaidi kufanya, ambacho kitamfanya asahau ugumu aliokutana nao.

Mitandao ya kijamii inaleta raha ya muda mfupi, kutokana na yale mtu anayoona, hasa maisha ya wengine. Lakini hili linamzuia mtu kupata kile anachotaka, kwa sababu anakuwa ameacha kufanya anachotaka kufanya.

SOMA, NG’ANG’ANA NA KATAA; Njia Pekee Ya Kuweza Kufanya Makubwa Kwenye Zama Hizi Za Usumbufu Wa Hali Ya Juu.

Na hata ukiamua kuondoka kwenye mitandao ya kijamii, bado unapata njia za kupoteza muda. Kwa sababu wapo wengi ambao hawapo kwenye mitandao ya kijamii au hawaendi huko wanapokutana na changamoto, lakini bado wanapoteza sana muda.

watu wamekuwa wanapoteza muda kabla hata ya kuja kwa mitandao ya kijamii, watu wamekuwa wakitafuta vitu rahisi kufanya pale wanapokutana na changamoto mbalimbali.

Hivyo ili kuweza kufika pale tunapotaka, ili kuweza kuepuka mitandao ya kijamii kuwa mtego kwetu, tukae kwenye kile ambacho tumepanga kufanya. Kama umepanga kufanya kitu fulani kwa muda fulani, kaa kwenye kitu hicho mpaka muda huo uishe, hata kama unaona hupati cha kufanya.

SOMA, #KURASA_KUMI ZA KITABU LEO; Ndani yetu tuna kitu kikubwa, tumekamilika na tuna kila tunachohitaji.

Zoezi hili litaifundisha akili yako nidhamu ya kuwa kwenye kitu kimoja. Kwa sababu mpaka sasa huenda umeshaharibu nidhamu hiyo hivyo huna tena uwezo wa kukaa kwenye kitu kimoja.

Kazana kuepuka kila aina ya usumbufu, kuweka mazingira yanayokuwezesha wewe kufanya ulichopanga kufanya, na muhimu zaidi, kukaa kwenye hicho unachofanya, kwa muda uliopanga kufanya.

Hata mambo yanapokuwa magumu, usikimbie, kaa hapo, jifunze na ufanye.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog