Habari za leo rafiki yangu?

Ni matumaini yangu kwamba umeianza siku hii vyema kabisa, ukiwa na hamasa kubwa ya kwenda kuweka juhudi ili kupata matokeo bora.

Wakati wewe umeamka na hamasa hiyo ya kwenda kufanya makubwa, wapo ambao wameamka na hamasa ya kukurudisha wewe nyuma, na cha kusikitisha zaidi ni kwamba watu hao ni wa karibu sana kwako, watu ambao unawaamini sana.

Watu wengi wamekuwa wanalalamika jinsi ambavyo wanarudishwa nyuma na watu wengine, mtu anakuwa amefanya jambo kwa nia njema, lakini watu wanalitumia kumrudisha nyuma. Ni rahisi kuona watu hawa ni wabaya, lakini hatupendi kukubali kwamba sisi wenyewe ndiyo tunawabeba.

Leo nataka tukaangalie ukweli kuhusu wale ambao wanaturudisha nyuma, uone jinsi ambavyo wewe mwenyewe unachagua kuwabeba halafu wao wanakudhuru.

Kabla hatujaangalia kwa kina kuhusu watu hawa, kwanza nikupe mfano ambao kila nikiufikiria, naona jinsi wengi tunafanya kosa hilo na linatugharimu.

Mfano huu ni hadithi fupi kati ya chura na ng’e. Chura alikuwa ng’ambo ya mto akitaka kuvuka kwenda upande wa pili ili kupata chakula. Akiwa pale ng’e akamjia na kumwambia chura ninataka kuvuka na kwenda ng’ambo ya pili ya mto, lakini siwezi kuvuka kwenye maji haya. Kwa kuwa na wewe unavuka, basi naomba unibebe mgongoni ili na mimi niweze kuvuka.

chura na ng'e

Chura akakataa haraka sana, akasema hilo haliwezekani, wewe ni ng’e na ng’e huwa wanauma. Nikikubeba kwenye mgongo wangu utaniuma na nitakufa kwa sumu yako.

Ng’e akamwambia nitakuwa mjinga kiasi gani kufanya hivyo, nikikuuma si tutazama wote? Siwezi kufanya hivyo, nisaidie rafiki yangu, niende nikapate chakula. Chura akafikiri kwa kina na kuona ni kweli, ng’e hawezi kufanya ujinga huo.

Basi akamwambia panda mgongoni twende. Ng’e akashukuru sana, akapanda mgongoni na safari ya kuvuka mto ikaanza, mambo yalienda vizuri mpaka pale walipofika katikati ya mtu, chura alisikia maumivu makali sana mgongoni, akamuuliza ng’e imekuwwaje tena umeniuma? Ng’e akajibu kwa masikitiko, unajua mimi ni ng’e na ng’e huwa wanauma. Basi wakazama wote kwa pamoja.

Mfano huu unaonesha uhalisia wa maisha kwenye maeneo mengi mno.

Wapo watu wengi ambao tunajitoa kuwasaidia, kuhakikisha wanavuka pale walipo sasa na kufika sehemu bora, lakini katika kufanya hivyo wanakuumiza.

Chukulia mifano ifuatayo;

Una ndugu ambaye hana kazi, ukaone umfungulie biashara, unaweka fedha zako na kuamini biashara hiyo itamtoa, baada ya muda unakuta biashara imekufa, na ana sababu kibao kwa nini kufa kwa biashara hiyo siyo kosa lake.

SOMA; ONGEA NA KOCHA; Waepuke Watu Hawa Kwa Nguvu Zako Zote, Wanakurudisha Nyuma.

Au una eneo la biashara au kazi, umeajiri watu ambao wanafanya kazi vizuri, akaja ndugu au rafiki yako ambaye hana kazi, akaomba umsaidie kumpa kazi ili maisha yake yaende. Unampa kazi japo hana vigezo vya kupata kazi. Lakini baadaye anafanya kazi chini ya kiwango mpaka wale wafanyakazi wengine wanakosa ile hamasa ya kazi walikuwa nayo mwanzoni.

Umewahi kuwa na mtu ambaye ulimsaidia kitu kipindi fulani, akawa alikuangusha, hakutoa matokeo uliyotegemea, mahusiano yakafifia na kila mtu akaenda na yake. Siku zikapita akaja tena akikuambia amebadilika, kipindi kile alikuwa hajayajua maisha, sasa hivi ameyajua na amejirekebisha. Akakuomba umsaidie tena, ukashawishika na kufanya hivyo, ukamsaidia lakini akakusumbua tena kama awali.

Yote hii ni mifano ya namna gani tunashawishiwa na ng’e ambao baadaye wanatuuma. Wanatuuma siyo kwa kutukomoa, bali kwa sababu ndivyo walivyo. Ng’e wanauma na hivyo watauma muda wowote wanapopata fursa hiyo.

Watu wana matatizo na changamoto zao, ambazo zinawarudisha wao nyuma, hivyo wewe unapohusiana nao, watakurudisha nyuma pia. Siyo kwa sababu wanataka kukukomoa, bali kwa sababu ndivyo walivyo.

Hivyo ili kuepuka hili, tunahitaji kufikiri kwa kina na kuacha kuendeshwa kwa hisia. Kwa sababu udhaifu wetu mkubwa kama binadamu upo kwenye hisia zetu, zinapokea mambo kwa urahisi sana na hisia zinapokuwa juu, fikra zinakuwa chini mara zote.

Kabla hujachukua hatua ya kumsaidia mtu, kwanza chukua muda wa kumchunguza na kuangalia kama kweli anaweza kufanya kile unachotaka kumsaidia. Kwa sababu wakati mwingine msaada wako ndiyo unamchochea mtu kuonesha tabia zake mbaya ambazo hakuwa na sehemu ya kuzionesha.

Na unapofanya uchunguzi wako huo, usimsikilize huyo unayemchunguza, bali angalia maeneo yote ambayo ameshapita au kufanya shughuli zake. Waulize watu waliofanya naye, alikuwa anafanyaje. Kama kwa namna yoyote ile alikuwa na tabia ambazo siyo za uaminifu, jua kabisa hata kwako ataonesha tabia za aina hiyo.

Njia nyingine ya kumjua mtu ambaye ukimsaidia au kushirikiana naye atakuumiza ni kumsikiliza anavyoongea. Ukiona mtu anamlaumu kila mtu ambaye amewahi kufanya naye kazi au shughuli yoyote, jua hapo yeye ndiye mwenye matatizo. Ukiona kushindwa kwake kupiga hatua anamrushia kila mtu kama sababu lakini siyo yeye, jua unajiandaa kuingia kwenye kulaumiwa.

Mwisho kabisa, unapochagua kufanya kazi au biashara na mtu yeyote ambaye una mahusiano naye nje ya biashara au kazi hiyo, kama ndugu, rafiki, jamaa na hata mwenza, basi unapaswa kuwa makini sana. Kwa sababu zile hisia zetu za mahusiano zinaweza kukuzuia kuona makosa ya wazi ya mtu huyo kwenye kazi au biashara mnayofanya.

Kwa kifupi, usifanye kazi au biashara na mtu ambaye hana uwezo kwa sababu tu unataka kumsaidia, utajiandaa kuanguka. Kwa sababu ndivyo alivyo, na alivyo kutakuwa na madhara makubwa kwako na kwa biashara au kazi yako.

Unapofanya maamuzi yoyote muhimu ya maisha yako, ambayo kushindwa kwa maamuzi hayo kutakuwa na madhara makubwa kwako, weka hisia pembeni na fikiri kwa kina.

SOMA; Ushauri; Ni Jinsi Gani Unaweza Kufikia Malengo Yako Kama Una Idadi Kubwa Ya Wategemezi?

Usiogope kusema neno hapana au kumpa mtu kitu kingine ambacho kitamsaidia zaidi. Kwa sababu wengi hupenda kusema ndiyo waonekane wana roho nzuri. Na hapo wanajiingiza kwenye matatizo na hata hiyo roho nzuri waliyotaka waonekane wanayo, haionekani pale matatizo yanapokuwepo.

MUHIMU; Kwa upande wa pili, kama wewe ni mtu ambaye umekuwa unasaidia kila mara lakini unawaangusha watu, unahitaji kubadilika. Kama kwa hapo ulipo una watu wa kuwalaumu kwamba ndiyo wamekufikisha hapo, basi jua wewe ndiyo tatizo, badilika, anza kuweka juhudi mwenyewe na watu wakiona juhudi zako watakuwa tayari kukusaidia. Kuanzia leo acha kabisa kusema kama isingekuwa fulani ningekuwa mbali, badala yake chukua hatua zitakazokufikisha kule unakotaka kufika.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

MIMI NI MSHINDI

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog