The key is to keep company only with people who uplift you, whose presence calls forth your best. – Epictetus

Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Ni siku mpya ya wiki mpya ambapo tumepata fursa ya kipekee ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya nakubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ZUNGUKWA NA WANAOKUFANYA UWE BORA…
Imesemwa sana kwamba sisi ni wastani wa watu watano wanaotuzunguka.
Kwamba tabia ulizonazo, hatua unazochukua na mafanikio uliyonayo, hayatofautiani sana na wale wanaokuzunguka.
Mnafanya vitu vinavyofanana.

Watu wanaokuzunguka, wale ambao unakaa nao kwa muda mrefu, iwe ni marafiki, wafanyakazi wenza, ndugu, jamaa na wengine wowote, wana ushawishi mkubwa sana kwako.
Wana nguvu ya kukufanya uchukue hatua au ukate tamaa.
Hii ndiyo maana ni muhimu sana uchague kwa umakini wale wanaokuzunguka.
Zungukwa na watu ambao ni bora zaidi kuliko wewe, watu ambao unawaangalia na kupata hamasa.
Zungukwa na watu ambao watakusukuma uwe bora zaidi, uchukue hatua na kusonga mbele.

Kuwa makini sana na watu unaoruhusu wawe karibu kwako, hakikisha ni watu ambao wanajua wapi wanakwenda na wanaweka juhudi kuwa bora zaidi.
Ikiwa ni watu ambao wapo wapo tu, ambao hawaamini wanaweza kufanya makubwa, watakukatisha tamaa na hutaweza kufanya makubwa.

Asubuhi ya leo tafakari ni aina gani ya watu wamekuzunguka,
Ni watu gani wa karibu zaidi kwako.
Angalia maisha yao na yako kama hutaona hayatofautiani sana.
Tafakari kule unakokwenda na angalia watu gani wameshafika kule unakoenda, au wapo njiani kwenda huko.
Na hawa ndiyo watu sahihi kwako kuzungukwa nao.
Kama huwezi kuwapata kwa karibu, basi jifunze kupitia waliopita au waliopo mbali, kwa kusoma vitabu vyao wu vitabu vinavyowahusu.

Nakutakia siku bora sana ya leo rafiki, uzungukwenna watu bora, wanaokusukuma uwe bora zaidi.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa