Kila mtu katika wakati fulani wa maisha yake, ameshawahi kuwa na ndoto kubwa sana za maisha yake. Ukianza na zile za utoto kwamba ukiwa mkubwa unataka kuwa nani, zipo nyingi ambazo watu wanaendelea kuwa nazo.
Wanakuwa na malengo na mipango ambayo ni mikubwa, yenye manufaa kwao na kwa wengine pia.
Lakini kama wote tunavyojua, mipango ni mipango na inapokuja kwenye utekelezaji, mambo huwa hayaendi kwa urahisi kama tunavyopanga. Hapo ndipo wengi wanapokutana na vikwazo, kuanzia ndani yao na hata nje yao.
Vikwazo vinapokuwa vingi, wengi huamua kuachana na ndoto kubwa waliyokuwa nayo. Wengi huamua kuachana na ndoto hizo kubwa, na kukubali kwamba maisha waliyonayo yanawatosha.

Hakuna ubaya wowote kwenye kukubali maisha ambayo mtu unayo, kila mtu anapaswa kukubali maisha yake. Ubaya unakuja pale unaposhusha viwango vyako, pale unapoachana na ndoto yako kwa sababu ya changamoto yoyote ile, hapo unakuwa umechagua kushindwa.
SOMA; UKURASA WA 854; Acha Kuzidisha Ugumu Wa Maisha Yako…
Unaposhusha viwango vyako, kwa sababu yoyote ile, unakuwa umechagua kushindwa, unachagua kujirudisha nyuma, na unakuwa umeupa uzembe nafasi, uzembe ambao upo ndani yako.
Changamoto hazikosekani kwenye jambo lolote lile, lakini kuacha kwa sababu ya changamoto unakuwa umechagua kushindwa mwenyewe.
Unapokutana na vikwazo au changamoto, ndiyo wakati wa kuongeza juhudi zaidi, ni wakati wa kupambana zaidi, wakati wa kuweka juhudi kubwa na kukua zaidi.
Kamwe usishushe viwango vyako kwenye maisha, usipunguze ndoto kubwa ya maisha yako. Badala yake jisukume zaidi, weka juhudi zaidi katika kufikia ndoto yako. Viwango unavyojiwekea kwenye kazi zako, biashara yako, maisha yako, imani yako na hata mahusiano yako, usivishushe kwa sababu yoyote ile.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog