Kama ilivyo kwamba shilingi ina pande mbili, ndivyo kila kitu kwenye maisha kilivyo. Kuna pande mbili za kila kitu tunachofanya au kupitia kwenye maisha. Na wakati mwingine pande hizo zinaweza kuwa zaidi ya mbili.

Ni tabia yetu sisi binadamu kuangalia au kuegemea upande mmoja pekee. Tunapenda kuangalia ule upande ambao tunakubaliana nao, ule upande ambao unaendana na sisi. Tunapenda kukaa na kuchukua ule upande unaotufanya tuonekane tupo vizuri.

shilingi

Lakini kukaa na kukubali upande huo pekee hakutakusaidia, zaidi kutakudanganya na ushindwe kuchukua hatua sahihi kwa kile unachopitia au unachotaka.

Ukitaka kuwa mtu mwenye kuuona ukweli na kuweza kuchukua hatua sahihi, unapaswa kuangalia upande wa pili wa shilingi, kwenye kila jambo. Kila kitu, ukishajua uko upande upi, angalia pia upande wa pili na uangalie. Jiweke upande huo wa pili na hapo utajifunza mengi zaidi, utaona kile ambacho hukuweza kuona ulipokuwa upande mmoja unaoutaka wewe.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Usichanganye Falsafa, Chagua Moja Na Itumie Vizuri.

Jiruhusu kuondoka kwenye mazoea yako ya kufikiri na kuondoka kwenye upande wako ili uweze kuona hali au kitu kwa mtazamo wa tofauti na ulionao kwa wakati huo. Hii itakufanya uone kile ambacho ulikuwa hujaona na uweze kufikiri tofauti.

Hali yoyote unayopitia, mara zote fikiria upande wa pili wa hali hiyo, itakuwezesha kuchukua hatua sahihi kwenye hali hiyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog