Huwa ninaamini ya kwamba mtu akijua kwa kina jinsi ambavyo dunia inafanya kazi, atakuwa amepata ukombozi mkubwa sana. Hii ni kwa sababu, mtazamo ambao wengi wanao kuhusu dunia, siyo sahihi na unawazuia kuchukua hatua na kufanikiwa.

Kwa mfano wapo watu ambao wamekuwa wanalalamika kwamba dunia haina usawa, kwa kutumia neno maarufu, dunia haiko fair. Lakini ukiangalia hiyo dhana yao ya usawa ambao wanafikiri dunia haina, unapata mashaka kama kweli watu hao wanaelewa jinsi dunia inavyofanya kazi.

wp-image--1288404680

Kitu cha kwanza kabisa na cha kusikitisha ambacho kila mmoja wetu anapaswa kujua ni kwamba dunia haijali kuhusu uwepo wako hapa duniani. Kwanza haijui hata kama upo, na uwepo wako hauna msaada wowote kwa dunia kama dunia. Hivyo kusema dunia haina usawa, wewe ndiyo unakuwa hauna usawa. Kwa sababu dunia umeikuta, na unaitegemea zaidi dunia kuliko inavyokutegemea wewe.

Sasa leo tunajifunza kitu kingine muhimu sana kuhusu dunia, kitu hicho ni kwamba, dunia haina upendeleo.

Kuna watu tukiwaangalia kwa nje, ni rahisi kusema wamependelewa, kwamba wamepata bahati kufika pale walipo. Ni rahisi kuona kama dunia imewapendelea na kuwapa vitu ambavyo hawakustahili kupata, wakati wewe unastahili lakini hupati.

SOMA; Usilalamike, Dunia Imekupa Kila Kitu, Ni Wewe Tu…

Ukweli ni kwamba, dunia inatoa kile inachopaswa kutoa, dunia inapima inachotoa kwa kutumia thamani. Utaona wenye fedha nyingi wanazidi kuwa nazo, wakati wasiokuwa nazo wanazidi kuwa na maisha magumu. Hii ni kwa sababu wenye fedha nyingi pia wanatoa thamani kubwa, na dunia haina namna, lazima ilipe thamani hiyo. Lakini wasio na fedha, unakuta hakuna thamani yoyote wanayokazana kuitoa na hivyo dunia haina deni kwao.

Dunia haijali unataka nini, dunia haijali unastahili nini, dunia inajali umetoa nini na inakulipa kadiri ulivyotoa. Inakurudishia kile ulichotoa, inalipa thamani kwa thamani. Haina upendeleo, inalipa kile inachopaswa kulipa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog