Kuna watu wanafanya biashara, na kuna watu wanataka kufanya biashara.
Kuna watu ni wakulima, na kuna watu wanataka kuwa wakulima.
Kuna watu ni waandishi, na kuna watu ambao wanataka kuwa waandishi.
Sheria ya kwanza ya mwendo ya Mwanasayansi Isaack Newton inasema kwamba kila kitu kitaendelea kuwa pale kilipo, iwe ni kwenye mwendo au kimesimama, mpaka nguvu ya nje itumike kukitoa kitu pale kilipo.
Na wale wanaofanya wanaendelea kufanya, na wanaotaka kufanya wanaendelea kutaka kufanya, mpaka pale mtu anapochukua hatua za makusudi za kutaka kubadili pale alipo sasa.
Kuna wafanyaji wachache sana ukilinganisha na wanaotaka kufanya, hii ni kwa sababu kufanya kuna changamoto zake, ambazo wengi hawapendi kuzifikia. Na kubwa zaidi, wanaotaka kufanya huwa wanasubiri mpaka wajione wamekamilika, ndiyo wawe tayari kuanza kufanya.

Chochote ambacho umekuwa unajiambia unataka kufanya lakini hufanyi, unasubiri nini usifanye? Chochote ambacho unajiambia unasubiri unajidanganya, ukweli pekee unaoweza kujiambia ni kwamba hujali kitu hicho, siyo muhimu sana kwako na hivyo ukifanya au usifanye hakuna tofauti kubwa.
SOMA; UKURASA WA 1032; Unajua Kabisa Wewe Siyo Mti…
Lakini kama kweli unajali kuhusu kitu, kama maisha yako umeyaweka kwenye kitu, utafanya. Hutaishia kutaka kufanya, utachukua hatua na kufanya. Na ufanyaji huo utakuwezesha kupiga hatua ukilinganisha na kutaka kufanya, ambapo hakutengenezi tofauti kubwa.
Kwenye jambo lolote ambalo unataka kweli kwenye maisha yako, jambo ambalo unajali sana, usiishie kuwa unataka kufanya, bali chukua hatua na fanya. Fanya, kuwa mfanyaji na siyo mtu anayetaka kufanya. Na popote unapokwama, zipo njia mbalimbali za kujikwamua mpaka ufike pale unapotaka kufika.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog