The mind unlearns with difficulty what it has long learned. – Lucius Annaeus Seneca
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya nakubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari INACHUKUA MUDA KUJIFUNZA KUACHA….
Kitu chochote ambacho mtu unafanya, ni kwa sababu ya tabia.
Unakuwa umejenga tabia ambazo zinayaendesha maisha yako.
Tabia hizi huwa zinachukua kudankujijenga, na pia zinachukua muda kuzivunja.
Hii ina maana kwamba, kama unataka kuacha kufanya kitu fulani ulichozoea kufanya, utahitaji kujifunza kuacha kufanya, kama ulivyojifunza kufanya.
Na zoezi hilo linachukua muda.
Watu wengi wamekuwa wanashindwa kupata mabadiliko ya kweli kwenye maisha yao kwa sababu wamekuwa wanataka mambo yatokee haraka.
Mtu amekuwa akifanya kitu kwa zaidi ya miaka 20, halafu anataka siku moja abadilike kabisa, aache kufanya kitu hicho na kufanya kipya. Hilo linashindikana na hivyo wanaona hawawezi kubadilika.
Chochote unachotaka kubadili kwenye maisha yako, jipe muda. Haitakuwa rahisi, utaanguka, utashawishika kurudi nyuma na mengine mengi. Lakini unapojua kwa hakika inakuhitaji muda kubadilika, utaweza kubadilika vizuri.
Nakutakia siku bora sana leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa