Maisha ni magumu kwa kila mtu, lakini kuna ambao maisha kwao yanakuwa magumu kuliko kwa wengine. Tofauti hii ya ugumu wa maisha baina ya watu, imekuwepo tangu enzi na enzi. Na haitokani na mahali mtu alipozaliwa wala hali aliyozaliwa nayo. Bali tofauti inatokana na maarifa ambayo mtu anayo juu ya maisha mazuri.

Wale ambao wana maarifa sahihi na wanayatumia kuboresha maisha yao, wamekuwa na maisha bora wakati wote. Lakini wale ambao wanakosa maarifa hayo, wamekuwa wakiwa na maisha magumu.

Pamoja na kwamba tunaishi kwenye zama za taarifa, zama ambazo ni rahisi kupata maarifa kuliko kipindi kingine chochote, wapo watu ambao wanaendesha maisha yao kwa mazoea. Wapo watu ambao hawajifunzi wala kuchukua hatua.

Tai Lopez, ambaye mjasiriamali na mwalimu wa biashara na mafanikio, walichukua hatua ya kujifunza kupitia vitabu na watu waliofanikiwa, na kugundua hatua 67 ambazo kila mtu akizipitia ataweza kuboresha maisha yake.

Tai anasifika kwa utaratibu wake wa kusoma kitabu kimoja kila siku, kitu ambacho kimemwezesha kusoma vitabu vingi na kupata maarifa mengi.

Mwandishi Troy Flora ambaye alihamasika sana na mafunzo ya Tai Lopezi, alikusanya hatua hizi 67 kwenye kijitabu hichi cha 67 STEPS, ambazo tunakwenda kujifunza hatua 20 kati ya hatua hizo 67 katika uchambuzi huu.

Karibu tujifunze, kuchukua hatua na kuweza kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa.

tai lopez

Zifuatazo ni hatua 20 kati ya hatua 67 za kukuwezesha kuwa na maisha bora.

 1. Tengeneza akili ya kibilionea. Huwezi kuwa na maisha mazuri kama huna maarifa mazuri unayoingiza kwenye akili yako. Jifunze kila siku kwa kusoma vitabu, kuhudhuria semina na mikutano, kuangalia video, kusikiliza vitabu na kila fursa inayojitokeza mbele yako ya kujifunza.
 2. Tengeneza mageuzi yanayokuwezesha kufanikiwa. Charles Darwin aligundua kwamba, viumbe hai wenye nguvu ndiyo walioweza kuishi na kuzaliana, wale waliokuwa dhaifu walikufa. Ili uweze kuwa na maisha mazuri, lazima uweze kutengeneza mageuzi ambayo yatakuwezesha kuendelea kuwepo wakati wote. Uwe tayari kubadilika, usibaki pale ulipo wakati wote.
 3. Kuwa mnyenyekevu. Jua kwamba huwezi kujua kila kitu, unahitaji msaada wa wengine kufanikiwa.
 4. Kuwa na mtu/watu ambaye unamwangalia na anakuhamasisha kuchukua hatua. Watu hawa wanaitwa mamenta, ni watu ambao watakuwezesha kupiga hatua kubwa zaidi ya ulipo sasa.
 5. Tofauti ya watu masikini na matajiri ni nidhamu. Wote wanapata fedha, matajiri wana nidhamu ya kudhibiti matumizi, kuweka akiba na kuwekeza. Masikini wanatumia fedha yote mpaka iishe, na wanaenda kukopa.
 6. Ondokana na mawazo ya bahati nasibu/kamari. Hakuna kitu kizuri kinachotokea kwa bahati na kwa haraka au njia ya mkato. Wapo ambao wamekuwa wakifikiria wanahitaji kushinda bahati nasibu au kamari ili wafanikiwe, dunia haifanyi kazi hivyo. Hata wanaoshinda bahati nasibu au kamari, haiwachukui muda, wanarudi kwenye umasikini.
 7. Ondokana na hali ya kuona kwamba huwezi. Tumefundishwa woga na kuona peke yetu hatuwezi, mpaka tufanyiwe kile ambacho wengine wamekuwa wanatufanyia. Unahitaji kuondokana na hali hiyo, na kujua kwamba una uwezo mkubwa wa kufanya makubwa. Utumie.
 8. Usizichukie jumatatu na kuzipenda ijumaa. Kwa maisha ya mafanikio, siku zote zinapaswa kuwa sawa. Lakini wasio na mafanikio, huchukia jumatatu na kuziita blue Monday na kuzipenda ijumaa na kuziita TGI (Thank God It’s Friday). Fanya kile unachopenda, ambacho utakifanya kila siku ya maisha yako.
 9. Unaweza kusoma kitabu kimoja kila siku. Kusoma vitabu ni njia ya kutengeneza timu yako ya washauri kwenye kila unachofanya. Tai Lopez amekuwa na utaratibu wa kusoma kitabu kimoja kila siku, kwa kutafuta yale maarifa muhimu ya kitabu na kukazana na hayo. Anasema vitabu vingi vina maelezo mengi ambayo huyahitaji, ukishajua unataka nini, ni rahisi kusoma vitabu vingi.
 10. Kugeuza makaa kuwa almasi. Almasi ndiyo kitu kigumu kuliko vitu vyote duniani, lakini inatengenezwa na makaa ambayo siyo magumu sana. kinachotokea ni makaa hayo kuwekwa kwenye presha kubwa mpaka yanakuwa almasi. Hivyo kama wewe unataka kuwa almasi, lazima upitie mazingira magumu, yanayokutengeneza na kukufanya kuwa bora zaidi.
 11. Jiandae kwa matokeo mabaya, lakini tegemea matokeo mazuri. Mara nyingi mambo hutokea kwenye maisha na kujikuta hatujajiandaa. Hii ni kwa sababu huwa tunafikiri kila kitu kitaenda kama tunavyotaka. Ukweli ni kwamba mambo hayaendi kama tunavyotaka sisi, bali yanaenda kama yanavyoenda yenyewe. Hivyo ni muhimu ujiandae kwenye lolote unalofanya, ili matokeo yakija mabaya, uwe na maandalizi, na yakija mazuri, ufurahie.
 12. Nguvu za asili. Jua kwamba kuna nguvu za asili, ambazo huwezi kuzivunja na ukabaki salama. Kama ambavyo ukipanda kwenye jengo refu na kujiachia lazima uanguke chini na uumie, japo ndege hawaumii kwa kufanya hivyo. Kila unachofanya, usilazimishe mambo ambayo yatakwenda kinyume na nguvu za asili. Mfano usitake kuanza biashara leo halafu kesho ikawa ina mafanikio makubwa, kila kitu kinachukua muda.
 13. Tengeneza mfumo bora wa kupanga mambo yako. Kupanga kuna faida kuliko kutokupanga. Lakini kupanga pekee hakuna msaada mkubwa. Unahitaji kuwa na mfumo wa mipango, ambapo unakuwa na mpango zaidi ya mmoja. Unakuwa na mpango wa mambo yakienda vizuri, unakuwa na mpango wa mambo yakienda vibaya, halafu unakuwa na mpango wa mambo yanavyoweza kwenda. Kwa kuwa na mipango hiyo mitatu, hutakwama pale mambo yanavyokwenda tofauti na ulivyotegemea.
 14. Tengeneza kundi la kukusaidia kufanikiwa. Hakuna mtu anaweza kufanikiwa kwa nguvu zake yeye mwenyewe, kila mtu anahitaji msaada wa watu wengi ili kuweza kupiga hatua kubwa. Unahitaji kuwa na kundi la watu ambao unawategemea na wanakusaidia kupiga hatua. Unahitaji kuwa na marafiki ambao wanakupa hamasa ya kupiga hatua na kukushauri vizuri. Unahitaji kuwa na kundi la washauri (mastermind) ambao wanakufuatilia kwa karibu kwa kila unachofanya. Pia unahitaji wasaidizi kwenye yale unayofanya.
 15. Zima ujinga wako. Watu wengi hufikiri wanajua sana kumbe hata hawajui, wengine wanaamini wapo sahihi zaidi kumbe hawapo sahihi. Ili uweze kujifunza, lazima ukubali kuzima ujinga wako. Lazima ukubali kwamba hujui ndiyo ujifunze, lazima ukubali kwamba huenda unakosea ili uwe sahihi. Ukiamini unajua na uko sahihi mara zote, utakuwa na ujinga wako milele.
 16. Kuwa mmoja kati ya mia moja. Allen Nation aliwahi kunukuliwa kusema siri ya mafanikio kwenye maisha ni kuwapuuza watu 99 kati ya watu 100 na kumsikiliza mtu mmoja. Tafuta yule anayekufaa, yule anayejua na anayekupa hamasa ya kupiga hatua, na msikilize huyo, wapuuze wengine kwa sababu huna muda, fedha wala nguvu za kumsikiliza kila mtu. Kwa upande wa pili, wewe pia unahitaji kuwa mmoja kati ya 100 wanaofanya kile unachofanya wewe, ukifanye kwa ubora na tofauti kubwa sana.
 17. Chagua eneo dogo unaloweza kulitumikia vizuri. Watu wengi wamekuwa wakifikiria kuanza na eneo kubwa, kuhudumia kila mtu na kuishia kushindwa kabisa. Chochote unachotaka kufanya, anza kulenga eneo dogo, chagua kikundi cha watu ambao utawatumikia vizuri, ambacho utatawala kwa kile unachofanya, na hapo utatengeneza mafanikio makubwa kuliko kutaka kumfikia kila mtu.
 18. Tengeneza makosa madogo na Kila mtu anakosea kwenye maisha, lakini kukosea kwenye mambo madogo na machache, kunakuwezesha kujifunza na kutokurudia makosa hayo. Kukosea kwenye mambo makubwa na mengi, kunaweza kukuondoa kabisa kwenye safari ya mafanikio. Kwa mfano kama hujawahi kuanza biashara kabisa si vyema kuchukua mkopo mkubwa na kwenda kuanza biashara, utakosea halafu utapata hasara kubwa. Badala yake unahitaji kuanza na biashara ndogo na kukua, utajifunza kupitia makosa madogo utakayofanya, ambayo hayataua kabisa biashara yako.
 19. Nguvu ya mawasiliano. Siyo unachosema, bali unakisemaje ndiyo kina nguvu. Unahitaji kutengeneza mawasiliano yenye nguvu, ambayo yatakuwezesha kufikisha ujumbe wowote ambao unataka uwafikie watu na waweze kuchukua hatua. Unapotoa ujumbe, wafikirie wale unaowapa ujumbe, na jua kitu gani kinawahamasisha kuchukua hatua. Kwa kujua hayo, utaweza kuwahamasisha kuchukua hatua.
 20. Kila mtu ashinde au usikubaliane kabisa. Kuna aina tatu za makubaliano, moja mmoja ashinde na mwingine ashindwe, mbili, wote washinde, tatu wote washindwe. Unapoingia kwenye makubaliano yoyote na mtu yeyote, hakikisha kila upande unashinda, kama hilo haliwezekani basi ondoka kwenye makubaliano hayo, hata kama wewe unashinda na upande mwingine unashindwa. Njia pekee ya kujijengea sifa bora na ushirikiano na wengine, ni kumwezesha kila mtu anayejihusisha na wewe kushinda.

Hizi ni hatua 20 kati ya hatua 67 zilizopo kwenye kitabu hichi. Hatua hizi nimezichagua bila ya mpangilio maalumu, hivyo ukisoma kitabu kizima, utazipata hatua zote 67.

Ni kitabu kifupi kusoma na ambacho ni rahisi kuondoka na vitu vya kwenda kufanyia kazi. Kitu kimoja muhimu sana kwenye kitabu hichi ni kujifunza na kuchukua hatua. Unapokuwa na maarifa sahihi na ukayafanyia kazi, huwezi kubaki pale ulipo sasa.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Usomaji

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz