Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza chanzo kikuu cha matatizo makubwa, je unakijua ni kipi? Karibu tujifunze.

Rafiki, kitu pekee ambacho hatuwezi kukisimamisha katika maisha yetu basi ni changamoto tunakutana nazo kila siku kwenye maisha yetu ya kila siku. Njia bora ni kujifunza kupitia changamoto tunazopitia kila siku, lakini pia kukabiliana nazo na siyo kuzikimbia.

41162-rt

Huwa tunapata changamoto mbalimbali lakini nyingine ni kubwa lakini nyingine huwa ni ndogo. Changamoto zinakuwa ni kama mawimbi katika bahari na hakika huwezi kuzisimamisha hata siku moja. Kila mtu aliyefanikiwa kupitia jambo fulani lazima alipitia katika changamoto fulani, lakini uvumilivu wake na kuzikabili na siyo kuzikimbia  ndiyo zimemsaidia kupata ushindi.

Lakini chanzo kikubwa cha matatizo makubwa ni matatizo madogo madogo ambayo tunayapata na kuyadharau. Kwa mfano mtu akiumwa tumbo hawezi kuchukua hatua  haraka matokeo yake lile tumbo linalomuumba linakwenda kuzaa matatizo mengine. Kama mtu akiamka na kujikuta anaharisha damu atachukua hatua haraka sana ya kwenda hospitali kumuona daktari na kupatiwa matibabu.

SOMA; Tatua Changamoto Hizi Mapema Ili Zisikuzuie Kufanikiwa.

Mpendwa msomaji, sisi binadamu tumekuwa ni watu wa kudharau sana mambo madogo madogo na kuyapa kipaumbele mambo makubwa. Haya madogo tunayoyadharu ndiyo yanazaa makubwa, tatizo la viporo vya kazi ulivyonazo vilianza na tatizo dogo la kuahirisha mambo matokeo yake yakasababisha matatizo makubwa. Leo ukiona ufa mdogo katika nyuma huwezi kuchukua hatua haraka lakini kumbe huo ufa mdogo ukiachwa ndiyo unaleta madhara makubwa.

Tunaalikwa samaki tumkunje angali mbichi maana yake tuanze kulikabili tatizo kabla ya halijawa kubwa. Usisubiri mpaka uwe na unene wa kupitiliza ndiyo uanze kufanya mazoezi na kupunguza vyakula vinavyosababisha uzito mkubwa. Usisubiri mpaka ufeli mtihani ndiyo uanze kusoma hapana anza sasa kabla hujafeli mtihani kwani kuchukua hatua mapema itakusaidia kuokoa mambo mengi.

Umekutana na mtu amekukwaza samehe hapo hapo, mfutie deni kabisa kuliko kuendelea kubaki  na uchungu matokeo yake uchungu  na maumizo unayoendelea kuyaweka yanakuja kukuletea mfadhahiko mkubwa. Baadaye unakuja kuwa na mafurushi makubwa ya mzigo au hustahili hata kuubeba yote haya ni kwa sababu ya kudharau tatizo dogo.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The 67steps (Njia Rahisi Ya Kuwa Na Maisha Mazuri).

Rafiki, tundu dogo katika meli linaweza kusabibisha meli kuzama kama halijatatuliwa mapema lakini kama likidharauliwa kadiri ya udogo wake lazima meli itazama tu.

Hatua ya kuchukua leo, najua unayo mambo mengi kama siyo matatizo madogo ambayo unayasogeza mbele kila siku badala ya kuyachukulia hatua leo. Kadiri unavyokwepa matatizo madogo ndivyo unavyokaribisha matatizo makubwa. Jifunze leo kuchukua hatua kwa tatizo dogo lolote unalolipata katika maisha yako ya kila siku.

Kwahiyo, huwa tunajipalilia matatizo makubwa sisi wenyewe katika maisha yetu, kitu ambacho tunaweza kukifanya sasa, tunataka tukifanye baadaye na kitu ambacho tunataka tukifanye leo tunataka tukifanye kesho na mwisho wa siku mwendo unakuwa ni kusogeza mbele hadi tatizo kubwa linakuwa. Chochote unachoweza kufanya sasa fanya, tatizo lolote dogo unaloweza kutatua litatue haraka kuliko kusubiri liwe kubwa.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana.