Kuna watu wanasema usifanye kazi kwa nguvu, fanya kazi kwa akili. Hawa ni wavivu ambao wanafikiri kuna njia rahisi ya mafanikio. Hata daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, mtu ambaye anakuwa amekaa darasani miaka mingi mpaka kufikia hatua hiyo, anatumia nguvu anapofanya upasuaji. Kwa sababu upasuaji mmoja unaweza kuchukua zaidi ya masaa 10.
Hivyo chochote unachofanya, jua ya kwamba nguvu na akili zinakwenda kwa pamoja. Lazima ujue vizuri sana kile unachofanya, na ujue njia za kufanya kwa ubora zaidi. Lakini muhimu sana, lazima ujue kwamba nguvu inahitajika. Lazima uweke nguvu katika kile unachofanya, ili uweze kuzalisha matokeo. Hata kama umeajiri watu, wewe unahitaji kufanya kazi zaidi hata ya wale uliowaajiri. Kwa sababu kile ni kitu chako, wewe ndiye wa kukijali zaidi.

Kitu kingine muhimu sana, ambacho kinaendana na hayo mawili ni kujitoa, kuwa tayari kuweka kila kinachopaswa kuwekwa ili kuweza kupata matokeo mazuri kwenye kile unachofanya. Hata kama upo tayari kuweka akili na nguvu, kama hujajitoa kweli, hutapiga hatua kubwa. Utaanza, utakutana na changamoto na utaishia hapo. Lakini unapokuwa umejitoa, kwamba ije mvua lije jua nitafanya, utafanya na utafanikiwa.
SOMA; UKURASA WA 959; Jitangazie Uhuru Huu Muhimu Sana Kwa Mafanikio Yako…
Mwisho, kujiamini wewe mwenyewe na kuamini kile unachofanya, hichi ndiyo kinakupa nguvu ya kuendelea kufanya, na kujitoa kwako kuwa na maana. Kama hujiamini kwenye kile unachofanya, hutakuwa na hamasa ya kukifanya. Kutokujiamini kutakunyonya nguvu zako zote, utataka kufanya lakini nguvu hakuna kabisa. Kama huamini kile unachofanya, hutaweza kujitoa kweli kukifanya. Unaweza kuwa na nguvu ya kufanya, ukaanza kufanya na ukakutana na changamoto, utaishia hapo haraka sana. Kwa sababu huna imani kwenye kile unachofanya.
Chochote unachofanya kwenye maisha yako, iwe ni kazi, biashara, kilimo, na hata mambo mengine ya kimaisha kama malezi, mahusiano unahitaji kuweka kazi hasa, unahitaji kuwa na maarifa sahihi ya kufanya, uweke nguvu katika kufanya, ujitoe kweli kufanya mpaka upate matokeo unayotarajia na ujiamini wewe mwenyewe pamoja na kuamini kile unachofanya. Kwa njia hii, hakuna atakayeweza kukuzuia kufanikiwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog