Watu wengi wanapoyaangalia mafanikio, huwa wanaangalia vitu vikubwa sana. Huwa wanaangalia nyakati ambazo mtu ameweza kupiga hatua kubwa sana kutoka kwenye hatua ndogo. Lakini mafanikio huwa hayapo hivyo.

Kwa mfano, hadithi nyingi za mafanikio huwa zinakupa kabla na sasa, au kama inavyotumika BEFORE na AFTER. Yaani mtu alikuwa hapa, na sasa yupo hapa. Sisi tunaona amepiga hatua kubwa kweli, na kwa mwonekano huo hatua ni kubwa.

Lakini huo siyo ukweli. Mtu ambaye alianza kuimba kwaya kanisani, na sasa ni mwanamuziki mkubwa, hakuruka tu moja kwa moja kutoka kwaya kanisani mpaka kuwa mwanamuziki mkubwa. Mtu aliyeanza na biashara ndogo na sasa anamiliki biashara kubwa, hakuruka kutoka biashara ndogo mpaka kubwa.

Maisha Bora

Upo mchakato ambao mtu alipitia, kuweza kutoka chini mpaka kufika juu, na mchakato huo huwa unahusisha vitu vidogo vidogo sana ambavyo vinafanywa mara kwa mara lakini huwezi kuviona. Mwanamuziki mdogo anayeandika na kuimba nyimbo kila siku kwa miaka 10 atapiga hatua kubwa sana. mfanyabiashara anayeanza na biashara ndogo, lakini kila siku anahakikisha anapiga hatua, baada ya miaka 10 anakuwa mbali sana.

Hii ina maana kwamba, mtu yeyote, kwa chochote anacho fanya, anayo nafasi ya kuweza kupiga hatua kubwa sana na kufanikiwa. Lakini tu, anahitaji kuacha kuangalia ule ukubwa wa mafanikio na kuyaangalia mafanikio kwa udogo wake.

SOMA; UKURASA WA 930; Dunia Haihitaji Mwongeaji Mwingine…

Njia bora ya kuyaangalia mafanikio kwa udogo na kuweza kuyafaidi, ni kutengeneza siku yako yenye mafanikio inaonekanaje. Wewe kazana na siku moja tu. Kwamba ili siku yako iwe na mafanikio, inabidi iweje; uamke mapema, ufanye shughuli zako, ujifunze, uongeze kipato, uongeze juhudi, udhibiti matumizi na mengine mengi.

Ukishaitengeneza siku yako moja ya mafanikio ikoje, hapo kazi inabaki moja tu, rudia siku hiyo kila siku, kila siku. Yaani kila siku hakikisha unaiishi ile siku yako ya mafanikio. Hakikisha kila unachofanya kila siku ni kile kinachozalisha siku ya mafanikio.

Kwa kukazana na siku hiyo moja, na kuweza kuirudia kila siku, iwe kuna mvua au kuna jua, kutakutengenezea mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako. Na watu nje watasema yule ana bahati, yule kaanza chini na sasa yupo juu. Kumbe ulichokifanya ni kuujua msingi wa chini kabisa wa mafanikio.

Itengeneze leo yako yenye mafanikio, kisha iishi leo hiyo kila siku ka siku zote za maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog